Na Eunice Lugiana, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amekutana na watumishi wa Kanda hiyo kwa ajili ya kupata ‘Iftar’ pamoja nao katika mfungo mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza wakati wa Iftar hiyo tarehe 22 Machi, 2024 iliyofanyika Mahakama Kuu-Dar es Salaam, Mhe. Maghimbi alisema funga mbili zimekutana kwa pamoja yaani funga ya Kwaresma na funga ya Ramadhani hivyo ameona ni vema kukutana kama Waislamu na Wakristo wakae kwa pamoja kama timu.
“Lengo la kukutana ni kukaa pamoja ili tuongee, tufurahi, tupendane na kuzoeana kisha tuendelee kuchapa kazi, lakini nawaomba sana baada ya leo tuendela kupendana tuwe na umoja tukisema kuna shughuli tuitikie sio tena tuanze kunyata,” alisema Jaji Mfawidhi.
Aidha akitoa salaam za shukrani, Mhe. Maghimbi alisema kwa sababu kazi zinakwenda hawana budi kukaa pamoja na kufurahi kwa pamoja akiahidi kuwa, wakati mwingine wataenda kwenye shughuli nyingine ambayo itawafanya kuwa pamoja na kufurahi.
Naye, Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Sundi Fimbo alimshukuru Mhe. Maghimbi na kukiri kwamba, kitendo hicho kimewaonesha ukarimu na upendo wa dhati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni