Na Jeremia Lubango na Lydia Churi-Dodoma, Dar es salaam
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Tume
ya Utumishi wa Mahakama imekuwa ni Taasisi ya kwanza kumpunguzia mwananchi
gharama katika suala la upatikanaji wa ajira nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa
Usaili wa Watumishi wa Mahakama uliofanyika jana katika maeneo mbalimbali
nchini akiwa katika kituo Jumuishi cha Utoajhi haki jijini Dodoma, Prof. Ole
Gabriel amesema Tume imekuwa ni Taasisi
ya kwanza kubuni utaratibu wa kutumia TEHAMA katika usaili wa awali yaani kabla
ya Msailiwa kufika kwenye hatua ya mahojiano ya ana kwa ana (Oral Interview).
“Matumizi ya mfumo wa Kielektroniki yameiwezesha
Tume kufanya Usaili kwa wakati moja katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo
kumpunguzia gharama anayefanya Usaili ambapo sasa hatalazimika kusafiri kutoka
eneo moja kwenye lingine kwa ajili ya kufanya usaili”, alisema Katibu huyo wa
Tume.
Alisema
tangu mwaka 2022, Tume iliona kuna umuhimu wa kutumia mfumo wa kielektroniki
katika mchakato wa ajira za Watumishi wa Mahakama kwa lengo la kupunguza
gharama, kuleta uwazi zaidi na kupunguza malalamiko kwa baadhi ya waombaji wa
nafasi za kazi zinazotangazwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Katibu
wa Tume alisema mwaka huo, Tume kwa kushirikiana
na Wataalam wa TEHAMA kutoka Mahakama ya Tanzania ilibuni na kusanifu Mfumo wa
maombi ya kazi “ JSC Recruitment portal” ili kufanikisha mchakato wa ajira za
watumishi wa Mahakama ya Tanzania.
“Mwaka
2022, Mfumo ulianza kutumika kwa majaribio na kuonesha mafanikio yakiwemo kupunguza malalamiko kwa baadhi ya
waombaji wa nafasi za kazi kazi, kupunguza muda wa mchakato wa ajira hadi
kufikia siku 45 Kutoka siku 90 za mfumo wa awali, kurahisisha uchambuaji wa
taarifa, Kuboresha Utendaji kazi na
kuwapunguzia gharama waombaji wa kazi kwa kufanya usaili mahali walipo au
karibu na maeneo yao”, alisema.
Aliyataja
maeneo ambapo usaili huo ulifanyika jana kuwa ni Arusha, Mwanza, Dar es salaam,
Tanga, Moshi, Kigoma, Iringa, Dodoma, Tabora, Shinyanga, Songea, Sumbawanga,
Morogoro, Mbeya, Musoma, Mtwara na Bukoba.
Mamlaka ya Tume ya
Utumishi wa Mahakama kama chombo cha kusimamia ajira na nidhamu za watumishi wa
Mahakama yanatokana na Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Toleo la mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Kifungu Na. 29 (1) cha Sheria ya
Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.
Sehemu ya Waombaji wa nafasi za Ajira ya Watumishi wa Mahakama Kada ya Hakimu Mkazi wakifanya Usaili kwa njia ya Kielekitroniki kwenye Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam. Zoezi la Usaili lilifanyika jana katika maeneo mbalimbali nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni