Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo amewaomba Wadau wa Haki Jinai kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Mifumo ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) iliyosimikwa ili kurahisisha huduma ya haki nchini.
Mhe. Kallomo alitoa rai hiyo juzi tarehe 22 Machi, 2024 wakati wa vikao vya kusukuma mashauri ya jinai na madai vilivyofanyika ndani ya ukumbi wa mikutano ulioko katika Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.
Vikao hivyo viliwashirikisha Wadau mbalimbali wa Sheria na Haki Jinai wakiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Polisi, Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wengine ambao ni wajumbe kwa mujibu wa sheria.
“Napenda kuwashukuru kwa kuwa chachu ya kuchangia haki kutendeka kwa jamii kwa wakati, ila nawakumbusha kuwa Mahakama ya Tanzania imehamia Mtandaoni na sasa tunafanya kazi zetu kwa uwazi. Nawaomba na nyinyi msiache kuwaelimisha wananchi juu ya Mifumo ya Mahakama na mtusaidie kufikisha elimu hii kwa wananchi,” alisema.
Mhe. Kallomo aliendelea kueleza kuwa kuna vipindi endelevu vya utoaji elimu ambavyo vinarushwa na Vyombo vya Habari vinavyotolewa na Mahakama ya Tanzania, ikiwemo Mahakama Kanda ya Morogoro.
“Elimu inaendelea kutolewa kwenye Vyombo vya Habari na kwa njia ya ana kwa ana kila siku ya Jumatano katika Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, hivyo mwananchi akiemilishwa ataweza kujihudumia na kufuatilia taarifa za shauri lake kupitia Mfumo wa Mahakama bila kufika mahakamani,” alisema.
Kupitia vikao hivyo, masuala mbalimbali yalijadiliwa na pongezi zilitolewa kwa Wadau hao baada ya kuwa wamefanikisha kutokuwa na mashauri ya mlundikano na kujadili namna bora ya kuendeleza hatua waliyofikia.
Akichangia hoja katika kikao hicho, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, ambaye ni Katibu, Bi. Veronica Chacha alieleza kuwa nguvu inayotumika kutolea maamuzi mashauri yaliyo katika hatari ya mlundikano ni vyema ikatumika pia katika mashauri yale mapya yanayofunguliwa ili tatizo litatuliwe mwanzoni.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro Mhe. Mary Kallomo (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao cha kusukuma mashauri ya jinai. Kushoto kwake ni Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Robert Kasele na kulia kwake ni Katibu wa kikao hicho kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wakili Veronica Chacha.
Wajumbe wa kikao cha kusukuma mashauri ya jinai Mahakama ya Wilaya Morogoro (juu na chini) ndani ukumbi.
Meza Kuu ikiongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo (katikakti), kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Robert Kasele na kushoto kwake ni Katibu wa kikao hicho kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Bi. Veronica Chacha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni