Jumatatu, 25 Machi 2024

JAJI MFAWIDHI SONGEA AHIMIZA USHIRIKIANO, UADILIFU KAZINI

Na Hasani Haufi- Mahakama Kuu Songea.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha amewaasa watumishi kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za Mahakama ili kutengeneza timu iliyo bora na yenye mafanikio.

Mhe. Karayemaha alitoa wito huo juzi tarehe 23 Machi, 2024 kwenye kikao cha Mahakimu wa Kanda ya Songea kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Chandamali uliyopo Manispaa ya Songea.

“Suala la utoaji haki kwa jamii, halimhusu Jaji Mfawidhi, Naibu Msajili au Mahakimu Wafawidhi katika ngazi ya Wilaya au Mkoa, bali watumishi wote wa Mahakama,” alisema.

Jaji Mfawidhi alisisitiza kwamba watumishi wote ni vema kutengeneza timu yenye kiu ya kupata mafanikio, kwani hata Mlinzi asipotekeleza jukumu lake kwa ukamilifu anaweza kupelekea haki ya mtu kuchelewa.

Mhe. Karayemaha aliwaasa kuwa Viongozi wazuri na imara kazini na sio kuwa sehemu ya kutengeneza au kuchochea kuporomoka kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji.

“Mkiondoka hapa nendeni mkawe Viongozi wazuri na imara wanaoimarisha uadilifu, weledi na uwajibikaji kwa watumishi na kuwaunganisha wote. Kiongozi bora ni yule anayesimama imara, asiyelaumu wala kulalamika. Kiongozi imara na bora pia ni yule anayetafuta suluhu ya changamoto na kuwa tayari kujifunza kwa wengine,” alisema.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele aliwakumbusha Viongozi hao kuzingatia maagizo, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamisi Juma wakati wa usikilizaji wa mashauri.

“Ningependa kuwakumbusha jambo dogo, lakini kubwa katika utekelezaji wa majukumu yetu, nalo ni kuzingatia miongozo na nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Jaji Mkuu na Viongozi wakuu wa Mahakama ya Tanzania,” Naibu Msajili aliwaeleza Mahakimu hao.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mhe. Japhet Manyama aliwakumbusha Kanuni za Maadili ya Maafisa wa Mahakama zinazowataka waishi katika misingi inayokubalika na kwa namna ipi wanapaswa kuishi katika maisha yao ya kila siku.

“Tukiwa kama Maafisa wa Mahakama tunatakiwa kuzingatia maadili yanayotuongoza tukiwa kazini, hata tukiwa nje ya eneo la kazi ili kuepuka kuingia katika shida zitakazopelekea kupewa onyo au kufukuzwa kabisa kazini,” Mhe. Manyama alisema.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akizungumza na Mahakimu waliohudhuria kikao hicho.


Wajumbe ambao ni Mahakimu (juu na chini) wakifuatilia kwa karibu mazungumzo ya Jaji Mfawidhi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (katikati waliokaa kwenye viti), akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Songea.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni