Jumatano, 13 Machi 2024

JAJI KAMUZORA AACHA ALAMA MOROGORO

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

 

Jana tarehe 12 Machi, 2024 ilikuwa siku ya furaha iliyochanganyika na huzuni miongoni mwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro wakati wa tafrija fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kumuaga Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Devotha Kamuzora aliyepata uhamisho kwenda katika Kanda ya Manyara.

 

Licha ya kufanya kazi ndani ya Kanda hiyo kwa kipindi kifupi toka alipohamishiwa akitokea Kanda ya Arusha mwezi Novemba 2023, Mhe. Kamuzora ameweza kufanya kazi kwa kushirikiana vizuri na Viongozi wake, watumishi wa Mahakama pamoja na wadau.

 

Hali hiyo imebaki kuwa kumbukumbu nzuri kwa watu aliowahi kufanya naye kazi ambao, katika tafrija hiyo, waliweza kuelezea matukio mbalimbali ya kuvutia wanayoyakumbuka.

 

Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Jaji wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Amir Mruma alimwelezea Jaji Kamuzora jinsi alivyokuwa mchapakazi na mwadilifu wakati wote,

 

“Tumekaa naye muda mfupi sana katika Kanda ya Morogoro kuanzia Novemba mwaka jana hadi leo, lakini uchapakazi wake mzuri na uadilifu sio kificho. Leo tumehamwa na dada, mama kwa wengine, mdogo wetu na mtoto wetu, huyu ni mtu muhimu kukaa naye karibu, ameenda Manyara lakini bado ni sehemu ya familia ya Mahakama,” alisema.

 

Mhe. Mruma alieleza baadhi ya matukio anayoyakumbuka ambayo Jaji Kamuzora aliwahi kuyatenda kwake kwa wema kipindi akiwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi  Manyara.

 

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni alisema wanashukuru katika kipindi chote walichofanya kazi pamoja na Mhe. Kamuzora, kwani amekuwa mlezi na amekuwa akitoa ushirikiano wakati wote na kujituma katika majukumu mbalimbali hata bila kuombwa kufanya hivyo.

 

Kwa upande wake, Jaji Kamuzora aliwashukuru wote kwa namna walivyoshirikiana naye wakati akiwa Morogoro na amepata malezi mazuri kutoka wa Jaji Mfawidhi, Mhe. Latifa Mansoor, ambaye alikuwa bega kwa bega naye wakati wa utekelezaji wa majukumu.

 

Alisema ushirikiano huo ulipelekea kufanya kazi kwa kujiamini na kutimiza majukumu yake kwa usahihi.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Devotha Kamuzora akizungumza wakati wa kuagana na watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro (hawapo kwenye picha).


 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma akitoa neno fupi wakati wa tafrija iliyoandaliwa kwa ajili ya kumuaga Jaji Devotha Kamuzora aliyehamishiwa Mahakama Kuu Manyara. 



Kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Devotha Kamuzora akishirikiana na Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng’eni (kushoto) kukata keki iliyoandaliwa kwa ajili yake.



 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Susan Kihawa akiongoza tafrija fupi ya kumuaga Jaji Devotha Kamuzora.


 


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Susan Kihawa (kushoto) akimlisha keki Jaji Devotha Kamuzora. Picha chini, akimkabidhi zawadi ya kitenge wakati  wa hafla hiyo.





Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro ikimsikiliza Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Devotha Kamuzora wakati wa hafla hiyo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni