Na Paul Pascal, Mahakama-Moshi
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi imefanya kaguzi za Mahakama za chini kuanzia ya Hakimu Mkazi na za Wilaya sita lengo likiwa ni kukagua shughuli zote za uendeshwaji wa Mahakama hizo.
Ukaguzi huo ni wa robo ya Tatu ya Mwaka wa Fedha 2023/2024. Akizungumza katika kikao na watumishi wa Mahakama za Wilaya Siha na Hai kwa nyakati tofauti Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt Lillian Mongella aliwapongeza watumishi wa Mahakama hizo kwa kazi ya kutoa haki.
“Tumejionea utendaji kazi wenu ni mzuri nimefurahishwa na taarifa ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya juu ya hali ya mashauri katika Wilaya hii niwapongeze wote kwa kuwa kazi ya kutoa haki sio nyepesi inahitaji ushirikiano wetu sote pia niwatake ndugu zangu kuhakikisha tunafuta utamaduni usio na tija wa kufanya vitu visivyo vya kimaadili,"alisema Mhe. Dkt. Mongella.
Alisema kuwa, ni lazima kila mtumishi kuwa muadilifu kwa kuwa wameaminiwa na kupewa nafasi wanazozitumikia, na kuwaasa kufanya kazi kwa weledi na uwajibikaji kwa kuwa kila mmoja ni mbobezi katika kada yake.
Kwa upande wa Mahakama za Wilaya Same, Mwanga na Rombo ukaguzi huo ulifanywa na Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi ambaye alisisitiza juu ya uwajibikaji na kujali afya ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi.
“Niwapongeze watumishi wote wa Mahakama hizi kwa kutimiza majukumu yenu ya msingi hali iliopelekea kuondokana na mashauri ya mlundikano katika Vituo vyenu, vilevile niwahimize watumishi wote kutenga muda wa kufanya mazoezi kwani mazoezi ni afya na ili kuwezesha utendaji uliotukuka hatuna budi kutunza na kujali afya zetu kwa hilo niwaombe muweke maanani na kutilia mkazo suala la mazoezi liwe ni miongoni mwa jukumu letu la msingi katika maisha yetu ya kila siku,” alisema Mhe.Kilimi.
Naye, Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzani, Kanda ya Moshi, Bi. Maria Itala alisema, “nipende kuwashukuru watumishi wote katika Wilaya hii kwa kuleta taswira chanya katika jamii tunayoihudumia hakika mmeitekeleza kwa vitendo nguzo namba tatu ya mpango mkakati wa Mahakama niombe ushirikiano zaidi ili zile kasoro ndogondogo zilizoonekana zisijitokeze na tushughulikie kwa pamoja.”
Ukaguzi uliofanyika ni ukaguzi wa kawaida kwa mujibu wa miongozo ya Ukaguzi kwa Mahakama ya Tanzania. Katika kaguzi hizo, Viongozi waliambatana na Majaji hao ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje, Mtendaji Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Bi. Maria Itala.
Ukaguzi huo ulianza tarehe 04 Machi, 2024 katika Wilaya za Same, Mwanga na Rombo ukiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi na baadaye tarehe 07 Machi, 2024 ukaguzi ulifanyika katika Wilaya za Siha na Hai ukiongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni