JAJI MFAWIDHI TANGA AONGOZA KIKAO CHA MENEJIMENTI
Na Mussa Mwinjuma-Tanga
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocati Mteule jana tarehe 20 Machi, 2024 aliongoza kikao cha Menejimenti cha Kanda kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Wilaya Korogwe wilayani Korogwe kilihudhuriwa pia na Majaji wa Mahakama Kuu kutoka katika Kanda hiyo, Mhe. Messe Chabana Mhe. Happiness Ndesamburo.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Naibu Msajili Mhe. Beda Nyaki, Mtendaji wa Mahakama wa Kanda, Bw. Humphrey Paya pamoja na watumishi wengine ambao ni wajumbe wa kikao hicho.
Kabla ya kikao hicho kuanza, Jaji Mfawidhi na ujumbe wake walitembelea na kukagua ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Korogwe na kujionea maendeleo ya jengo hilo la kisasa la Mahakama.
Pamoja na mambo mengi yaliyoongelewa katika kikao hicho,Jaji Katarina aliwakumbusha wajumbe kuhusu utoaji haki kwa wakati pamoja na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
“Sisi ndio wahusika wakuu kwenye jukumu la utoaji haki ndani ya Kanda ya Tanga, kazi yetu ni kuhakikisha haki inatendeka tena kwa wakati na ili tujue kama haki inatendeka, basi tuangalie idadi ya mashauri ya mlundikano,” alisema.
Jaji Mfawidhi alisisitiza kuwa majengo, mifumo na vitendea kazi vyote ni kuni kwa ajili ya kuivisha chakula ambacho ni umalizaji wa mashauri na haki kupatikana kwa wakati.
Katika kikao hicho, taarifa mbalimbali za kiutendaji na mashauri ziliwasilishwa kwa kila Wilaya na Mahakimu Wafawidhi ambapo ilibainiska baadhi ya Mahakama zilikua na mashauri ya mlundikano.
Kufuatia hatua hiyo, Jaji Katarina aliagiza mashauri yote ambayo yamechukua muda mrefu bila kumalizika sababu ziwekwe wazi ili hatua stahiki za haraka ziweze kuchukuliwa na haki ipatikane.
Aliahidi kutokua na mashauri ya mlundikano kwa upande wa Mahakama Kuu Tanga ndani ya kipindi kifupi kijacho.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Mteule (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Mradi. Kulia ni Naibu Msajili, Mhe. Beda Nyaki.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Mteule (katikati) akiongoza kikao hicho. Kulia kwake ni Jaji Messe Chaba na kushoto kwake ni Jaji Happiness Ndesamburo. Wengine ni Naibu Msajili Beda Nyaki (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Tanga, Bw.Humphrey Paya (aliyesimama).
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni