Na Mwinga Mpoli- Mahakama, Mbeya
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru amewasisitiza Mahakimu kuzingatia matumizi ya
mfumo wa Kielektronik wa Usimamnizi wa Mashauri (e-CMS) katika majukumu yao ya
kila siku na kuwataka kutambua kwamba, zoezi la matumizi ya mifumo hiyo ya
Mahakama halitarudi nyuma hivyo kila mmoja anatakiwa kuendelea kutumia mifumo
hiyo huku changamoto zingine zikiendelea kufanyiwa kazi.
Ameyasema hayo hivi karibuni katika kikao kazi
kilichofanyika Mahakama Kuu Mbeya, na kuwataka Mahakimu wafawidhi kufuatilia
matumizi ya mifumo hiyo katika vituo vyao kwa karibu. Kikao hicho kiliwajumuisha
Majaji, Manaibu Wasajili, na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wote wa Kanda ya Mbeya.
“Ni wajibu wa
kila Hakimu Mfawidhi kuhakikisha anasimamia na kufuatilia vyema matumizi ya
mfumo huu wa e-CMS katika kituo chake” alisema Mhe. Ndunguru
Aidha, Mhe. Ndunguru alisisitiza juu ya suala la kumaliza
mashauri ya muda mrefu, hasa yale ya utekelezaji wa hukumu za Mahakama
yaliyokaa muda mrefu Mahakamani pamoja na ukaguzi wa kina katika Mahakama zao.
“Ni vyema kukawa na mikakati thabiti ya namna ya
kumaliza mashauri ya muda mrefu lakini pia kila mmoja wetu achukue nafasi yake
na tuelezane ukweli pale penye changamoto. Zaidi tuhakikishe tunafanya ukaguzi
wa kina katika Mahakama zetu na tukague pia vyumba vya vielelezo na tuhakikishe
kila kielelezo kipo katika utaratibu unaotakiwa” alisisitiza Jaji Ndunguru
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa katika kikao hicho aliwapitisha Mahakimu Wafawidhi
kwenye takwimu za mashauri kwa mwaka 2023 kama ilivyokuwa imetolewa na kurugenzi
ya mashauri katika kikao cha Majaji Wafawidhi Arusha na kisha kujadiliana kwa
pamoja na kufanya tathmini ya utoaji haki kwa mwaka 2023 na kujiwekea mikakati
ya kumaliza mashauri yote ya mrundikano ifikapo June, 2024 lakini pia kuzuia
kabisa mlundikano wa mashauri kwa mwaka 2024.
Naye, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Mbeya Mhe. Aziza Temu alisisitiza juu ya kushiriki kikamilifu katika uandaaji
wa taarifa mbalimbali na zaidi wazikague taarifa hizo kabla ya kuzituma na wajenge
utamaduni wa kupitia barua pepe mara kwa mara kwani zinatumika kutoa maelekezo
mbalimbali ya viongozi.
Kikao kazi hicho kilitoka na maadhimio kadhaa ikiwemo
suala la umalizaji wa mashauri ya mlundikano, matumizi ya mifumo ya uendeshaji
wa mashauri na kubadirishana uzoefu katika masuala ya utekelezaji wa hukumu za
Mahakama.
Sehemu Majaji walioshiriki kikao kazi hicho,
katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru, (kulia) ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa na (kushoto) ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Emmanuel Kawishe.
Jaji wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa akiwapitisha washiriki wa kikao
kazi katika takwimu za mashauri mwaka 2023.
Sehemu ya Mahakimu Wakazi Wafawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya walioshiriki
kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni