Na. Innocent Kansha- Mahakama.
Jaji
wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)
Mhe. Dkt. Paul Kihwelo amefungua warsha ya maandalizi ya mtaala na miongozo ya
kufundishia mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi nchini leo
tarehe 5 Machi, 2024 katika ukumbi wa mikutano Protea Hotel jijini Dar es
salaam, warsha hiyo itafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 5 hadi 9
Machi, 2024.
Akizungumza
katika hafla ya ufunguzi wa warsha hiyo, Mhe. Dkt. Kihwelo amebainisha kuwa
uandaaji wa mtaala na miongozo ya kufundishi namna bora ya kuendesha mashauri
ya uchaguzi ni matokeo ya mkutano wa tarehe 12 Desemba, 2023 hadi tarehe 14
Desemba, 2023 jijini Arusha ulizaa makubaliano ya awali “Memorandum of Understanding
(MoU)” ya kuandaa mtaala na miongozo hiyo.
“Ningependa
kudokeza kwamba Mkataba wa Makubaliano (MoU) ushirikiano kati ya IJA na IFES ni
ushuhuda wa kile kinachokwenda kufanyika katika warsha hii, uandaaji wa mtaala
na miongozo ya kufundishia ni mojawapo ya ushirikiano mahususi ambao umeleta
maendeleo makubwa ndani ya kipindi kifupi iwezekanavyo”, ameeleza Jaji Kihwelo.
Mhe.
Kihwelo amesema, Mtaala na Miongozo hiyo ya kushulikia migogoro ya uchaguzi inaandaliwa
kwa pamoja na wataalum kutoka Mahakama ya Tanzania, Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) na Taasisi ya Kimataifa inayojishughulisha na Mifumo ya
Uchaguzi (IFES).
Mtaala
na Miongozo ya kufundishia mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya
uchaguzi kwa ajili ya Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu utaenda sambamba na
kuwanoa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakimu wa Mahakama za
Hakimu Mkazi na Wilaya nchini, amesema Jaji Kihwelo.
“Pia
ninajivunia sana timu ya wataalamu ambayo tumekusanyika pamoja kuandaa mtaala
na miongozi hii, inayojumuisha Majaji, Mahakimu na Wadau wengine muhimu wa kimataifa
wa maendeleo hapa nchini. Ushiriki imara, mchango wenu na kujitolea kwa kazi hii
adhimu hauna kifani. Wengi wetu tumelazimika kuacha shughuli zenu adhimu ili kujiunga
kwa zoezi hili maalum. Tunathamini sana uzoefu na utaalamu tulionao
tunapotekeleza jukumu hili adhimu”, amesisitiza Mhe. Kihwelo.
Jaji
Kihwelo ameongeza kuwa, azimio la pamoja la kupata mtaala bora na machapisho
ama nyenzo za mafunzo ya kufundishia namna bora ya utatuzi wa migogoro ya
uchaguzi vitakavyoendana na kusawili utendaji wa Mahakama ya Tanzania ni muhimu
kwa mchakato wa kidemokrasia kupitia haki ya uchaguzi ni msingi wa amani na
usalama kwa taifa lolote la kidemokrasia lenye thamani utawala wa sheria.
Jaji
Kihwelo ameushukuru Uongozi wa Mahakama kipekee Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa uongozi wake wa kimaono na usaidizi wake. Hakika
umekuwa chanzo cha msukumo ambao bila hiyo Taasisi isingefika hapo ilipo.
“Ni
kutokana na maono ya uongozi wa Mahakama kwamba, mtaala, miongozo na nyenzo za kufundishia
mafunzo ya namna bora ya kushughulika mashauri ya uchaguzi ambazo zinaandaliwa
na Wataalamu wa Mahakama, IJA na IFES zitakapo kamilika na hatimaye mafunzo
yatakayoendeshwa siyo tu yatakuwa yakizingatia Mahakama pekee bali pia yataakisi
umiliki na udhibiti wa Mahakama. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana siku zote
tumeifahamisha Mahakama kuhusu maendeleo yaliyofikiwa katika kila ngazi”,
ameongeza Mhe. Kihwelo.
Kwa
upande wake, Afisa Demokrasia, Haki na Utawala Bora kutoka Taasisi ya Kimataifa
ya Misaada ya Watu wa Marekani nchini, Bw. Stephen M. Andoseh amesema kuwa,
uandaaji wa mtaala, na miongozo ya kufundishia namna bora ya kuendesha mashauri
ya uchaguzi utasaidia kuondoa changamoto na kujenga mfumo imara wenye mafanikio
hasa kipindi cha uchaguzi na kuwasaidia maafisa wa Mahakama kutenda haki
kulingana na viapo vya kazi hiyo maalum. Maboresho hayo muhimu yatakayosaidia kwenye
utendaji kazi wa utatuzi wa migogoro ya uchaguzi nchini na nyaraka muhimu kwa
ajili ya rejea kwa maafisa wa Mahakama kwa upande wa Tanzania.
“Natambua
mwaka huu na mwaka ujao Tanzania itafanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba, uamuzi
wa kuandaa mtaala na miongozo ya kufundishia maafisa wa Mahakama namna bora ya
kuendesha mashauri ya uchaguzi, kwani Marekani ni mshirika mkubwa wa demokrasi
na tunaamini mwanachi ana haki ya kuchagua kiongozi anayemtaka”, amesema Afisa
huyo.
Afisa
Andoseh amesema, mchakato wa uchaguzi siyo jambo la kawaida, inatakiwa watu
kujidhatiti, kutekeleza kwa dhati, kulinda amani na haki za msingi na kufurahia
mchakato mzima, ndiyo maana ya umuhimu wa warsha mnayokwenda kuitekeleza. Hii
inamaanisha maafisa Mahakama ni walinzi muhimu wa demokrasia kutokana na viapo
vyao vya kuimarisha na kulinda utawala wa sheria.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akizungumza na kikosi kazi cha kuandaa mtaala na miongozo ya kufundishia mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi nchini katika ukumbi wa mikutano Protea Hotel jijini Dar es salaam leo tarehe 5 Machi, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni