Jumanne, 5 Machi 2024

MKUTANO WA KIMATAIFA UGANDA KUHUSU USULUHISHI WAANZA

Jaji Mkuu wa Tanzania kuongoza jukwaa kujadili utatuzi mbadala migogoro ya kimazingira

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kampala

Makamu wa Rais wa Uganda, Mhe. Jessica Alupo leo tarehe 5 Machi, 2024 amefungua Mkutano wa Kimataifa unaofanyika jijini hapa kuwaleta pamoja Viongozi mbalimbali wa Mahakama katika Bara la Afrika kukazia matumizi mbadala ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Wakati wa Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika katika Hotel ya Mestil, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma atakuwa miongoni mwa Viongozi wa Mahakama Afrika kuongoza jukwaa litakalojadili utatuzi mbadala wa migogoro ya kimazingira na katika sera za umma.

Akizungumza wakati wa kufungua Mkutano huo, Mhe. Jessica, ambaye alimwakilisha Rais wa Uganda, Mhe. Yoweli Kaguta Museveni, amesema mfumo wa kisasa wa haki una mengi ya kujifunza na kuiga kutoka kwenye dhana ya haki ya Kiafrika.

Amesema kuwa mbinu za kitamaduni za utatuzi wa migogoro kama vile upatanishi, uamuzi, upatanisho na mazungumzo ambayo Waafrika walitumia zamani zilikuwa na matokeao chanya katika uwepo kwa amani na uhusiano wenye usawa.

“Serikali ya Uganda inaiunga mkono Mahakama kupanua matumizi ya utatuzi mbadala ili kusaidia kufufua mifumo ya kitamaduni ya utatuzi wa migogoro,” amesema.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo emeeleza umuhimu kwa wadaawa kutumia njia ya usuluhishi katika kutatua migogoro kwenye muktadha mzima wa utoaji haki na kuomba kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ili kuunga mkono utaratibu huo.

Amesema kuwa mfumo rasmi wa umalizaji wa mashauri ukitumika kama njia pekee ya kutatua migogoro hautaweza kufikisha haki kwa wakati na haraka inayotarajiwa na wananchi.

“Kama mtangulizi wangu alivyokuwa anasema, hata Maafisa wa Mahakama wataamua kusikiliza mashauri kwa siku zote kwa wiki kuanzia Jumatatu hadi Jumapili wasingeweza kumaliza mashauri yote bila,”Jaji Mkuu wa Uganda amesema. 

Akasisitiza kuwa wanapaswa kuwekeza katika mafunzo na kusaidia mitandao ya njia mbadala ya utatuzi wa migogoro inayojumuisha Wapatanishi, Wasuluhishi na Mawakili ambao wanaweza kuendeleza mbinu bora kila wakati.

“Juhudi za kujenga uwezo zijumuishe mafunzo ya wataalamu wa sheria, viongozi wa kidini na serikali za mitaa, mamlaka za kimila, maafisa wa uchaguzi, polisi na maafisa wa usalama na mashirika ya haki za binadamu. Tuko hapa kujadili mada hii muhimu na kutoa mapendekezo yanayofaa kwa mustakabali wa njia mbadala katika kutatua migogoron barani Afrika,” amesema.  

Mhe. Owiny-Dollo ameeleza kuwa jitihada za kurejesha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala haziko mbali, kwani Nchi kubwa zaidi kiuchumi duniani, ambayo ni Marekani imegundua hili kwa muda mrefu. 

Amebainisha kuwa katika Nchi hiyo, asilimia 98 ya migogoro yote inasuluhishwa kwa njia mbadala na ni asilimia mbili tu inayoenda kwenye Mahakama rasmi za sheria.

“Vile vile, asilimia 95 ya migogoro yote ya jinai hutatuliwa kupitia usuluhishi na asilimia tano iliyobaki hutatuliwa kupitia mfumo wa kawaida wa Mahakama. Ndugu zangu, hii ndiyo njia sahihi tunayopaswa kupitia,” amesema.

Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu ameongozana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma na Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kituo hicho, Mhe. Isaya Arufani.

Viongozi wengine wa Mahakama wanaohudhuria Mkutano huo wa siku mbili ni Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Venance Mlingi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando na Afisa Itifaki, Bw. Juma Mshana.

Mkutano huo unaowaleta pamoja Majaji, Wahusika Sekta Binafsi, Mawakili wa Kujitegemea, Wasomi na Waendesha Mashtakana umeandaliwa na Mahakama ya Uganda kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Pepperdine kilichopo California Marekani. Kauli mbiu ya Mkutano huo ni Kurekebisha Utawala wa Haki katika Bara la Afrika.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akiwa katika Mkutano wa Kimataifa unaofanyika nchini Uganda kujadili njia mbadala wa kumaliza migogoro kwa njia ya usuluhishi.

 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kulia) akifuatilia yale yaliyokuwa yanajiri wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo.

Viongozi wa Mahakama ya Tanzania (juu na nchini) wakiwa katika Mkutano huo na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Isaya Arufani, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma, Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Venance Mlingi na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando.



Makamu wa Rais wa Uganda, Mhe. Jessica Alupo akizungumza wakati anafungua Mkutano huo.

Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kulia) akiwa Katina picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali, akiwemo Makamu wa Rais wa Uganda, Mhe. Jessica Alupo (wa tatu kutoka kushoto walioketi).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni