Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kampala
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 4 Machi, 2024 amewasili nchini Uganda kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa unaozihusisha Mahakama Afrika utakaojadili njia mbadala ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Mhe. Prof. Juma na ujumbe wake amewasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Entebe majira ya saa 7.30 mchana na kupokelewa na Jaji wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Patience Rubagumya na Afisa mmoja kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda, Lucas Mayanga.
Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu ameongozana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma na Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kituo hicho, Mhe. Isaya Arufani.
Viongozi wengine wa Mahakama wanaohudhuria Mkutano huo wa siku mbili ni Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Venance Mlingi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Augustina Mmbando na Afisa Itifaki, Bw. Juma Mshana.
Ujumbe huo wa Mahakama ya Tanzania unahudhuria Mkutano huo utakaofanyika kuanzia kesho tarehe 5 Machi, 2024 katika hoteli ya Mestil jijini hapa kufuatia mwaliko alioutoa Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo.
Mkutano huo umeandaliwa na Mahakama ya Uganda kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Pepperdine kilichopo California Marekani. Kauli mbiu ya Mkutano huo ni Kurekebisha Utawala wa Haki katika Bara la Afrika.
Katika Mkutano huo kutakuwepo na mjadala mpana kuzungumzia dhana mpya ya utatuzi wa migogoro barani Afrika kulingana na tafakari kwamba kile kinachoainishwa leo kama Utatuzi Mbadala wa Migogoro ndio msingi wa falsafa na utaratibu wa utatuzi wa migogoro barani Afrika.
Mkutano huo utawaleta pamoja Majaji, Wahusika Sekta Binafsi, Mawakili wa Kujitegemea, Wasomi na Waendesha Mashtakana kutoa fursa kwa Mahakama na watendaji wengine wa haki barani Afrika kufikiria upya upatanishi na uwekaji wa Utatuzi Mbadala wa Migogoro kama njia kuu, kama sio njia ya msingi ya kusuluhisha migogoro katika robo ijayo ya karne ya 21.
Zaidi ya hayo, Mkutano huo utaangazia mwelekeo unaoibuka, maendeleo na ubunifu kwenye Utatuzi Mbadala wa Migogoro katika kuimarisha upatikanaji wa haki na utatuzi wa haraka wa migogoro.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni