Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Arusha
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amesema Mahakama itaendelea kuimarisha uwazi
na uwajibikaji katika utoaji wa huduma zake.
Akifunga mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo wakufunzi wa Kamati za
Maadili za Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya ambao ni Majaji Wafawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Siyani amesema uwazi na uwajibikaji ni mambo
yatakayosaidia kujenga imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.
”Umma unayo haki si tu ya kusikia hatua zinazochukuliwa
dhidi ya vitendo visivyokuwa vya kimaadili dhidi ya Maafisa Mahakama bali pia
kuona namna hatua hizo zinavyochukuliwa”, alisema Kamishna huyo wa Tume.
Alisema ni matarajio ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na
Mahakama kuwa, elimu waliyopatiwa Majaji hao itakuwa ni chachu katika kuongeza
uwajibikaji na utendaji kazo wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa
na wilaya.
Jaji Kiongozi aliwakumbusha Majaji umuhimu wa kujenga na
kusimamia maadili ya Maafisa Mahakama na watumishi wengine wa Mahakama kwa kuwa
kazi ya Mahakimu ni lazima iendane na maadili ndani yake.
”Maadili kwa Maafisa Mahakama ni chemchemi ya ustawi wa
haki, uadilifu kwa Mahakimu na Majaji huzaa imani kwa wananchi, hakuna haki
bila imani na hakuna imani bila uadilifu”, alisema.
Alisema Kamati za Maadili zilianzishwa ili kuhakikisha
Maafisa Mahakama wanatimiza wajibu wao kwa uadilifu na endapo kamati hizo
hazitafanya kazi ipasavyo jamii itapoteza imani kwa Mhimili wa Mahakama.
Aliongeza kuwa kutoaminika kwa Mahakama kutasababisha
hukumu zinazotolewa kutoheshimika na hivyo wananchi hawataona umuhimu wa
kutumia Mahakama kama chombo rasmi kilichokasimiwa mamlaka ya kutoa haki.
Alisema Majaji wanayo kazi na wajibu wa kuendelea
kuimarisha usimamizi wa maadili kupitia vyombo mbalimbali zikiwemo kamati za
Maadili za mikoa na wilaya.
Alitoa wito kwa Majaji hao kutoa ushirikiano unaostahili
kwa kamati za maadili zinapotekeleza majukumu yake kila inapohitajika kwani
kutotimiza wajibu kwa kamati hizo ndani ya muda uliowekwa kunaweza kuzikwamisha
kamati hizo kutekeleza jukumu lake la kusimamia maadili ya Maafisa Mahakama.
Tume ya Utumishi wa Mahakama iliandaa mafunzo ya siku
mbili kwa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka maeneo mbalimbali
nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo Majaji hao kwenda kutoa mafunzo
yanayofanana (equal standard) kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa
Mahakama za Mkoa na Wilaya katika mikoa yote nchini.
Tume
ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia
uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili
kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la
kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na
majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu 29 cha Sheria ya Usimamizi wa
Mahakama Na.4 ya mwaka 2011.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani akifunga mafunzo ya siku mbili ya Majaji Wafawidhi yaliyolenga kuwajengea uwezo ili wawe wakufunzi wa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kwenye kanda zao yaliyofanyika jijini Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni