Na Christopher Msagati- Mahakama, Manyara
Mahakama
Kuu Manyara imefanya Ukaguzi katika Robo ya kwanza ya Mwaka 2024 kuanzia tarehe
25 Machi, 2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Mbulu, Hanang, Mahakama za Mwanzo pamoja
na Magereza ya Wafungwa na Mahabusu katika Wilaya hizo.
Azungumza
kwa nyakati tofauti wakati wa ukaguzi huo Mahakama ya Wilaya ya Mbulu, Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora aliwapongeza
watumishi wa Wilaya hiyo kwa utendaji kazi mzuri unaochangia mafanikio ya Kanda
nzima hususani kwa kumaliza mashauri kwa wakati na kupunguza malalamiko ya
wadaawa wanaofika Mahakama kila siku.
“Kwa
kweli kazi mnayofanya ni kubwa na mafanikio yanaonekana, kwa kipindi hiki
tunaona kuwa mashauri yanaenda kwa kasi na jambo hili limepunguza hata idadi ya
Mahabusu katika gereza. Hili linaenda sambamba na upunguaji wa malalamiko
katika Ofisi zetu,” aliongeza Mhe. Kamuzora.
Zoezi
hilo pia, lilifanyika katika Mahakama ya Mwanzo Endagkot na Gereza la Wilaya ya
Mbulu. Akizungumza wakati wa zoezi la ukaguzi wa gereza la Wilaya ya Mbulu, Kaimu
Mkuu wa Gereza la Mbulu Bw. Erick Pallangyo alipongeza uamuzi wa Mahakama wa
kufika Gerezani hapo na kusikiliza matatizo ya mahabusu na wafungwa ambao
wachache wao wanasubiri kupatiwa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri yao
ili wawaeze kukata rufaa za mashauri yanayowakabili kwa wakati. Mahakama kupitia
ujumbe huo uliahidi kulifanyia kazi jambo hilo ndani ya muda mfupi kupitia Uongozi
wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu.
“Mheshimiwa
Jaji ujio wako umeturahisishia kupata majibu ya maswali ambayo yalikuwa
yanaulizwa mara kwa mara na wafungwa na maabusu wa gereza hili ni matumaini
yetu kuwa kila mtu ameridhika kutokana na majibu na maelezo ambayo mmeyatoa”,
alisema Bw. Pallangyo.
Akiwa
katika ukaguzi wa Mahakama ya Wilaya ya Hanang na Mahakama ya Mwanzo Katesh,
Mhe. Kamuzora alikutana na changamoto ya mahabusu kutokupelekwa Mahakamani kwa
wakati, ikiwa ni kwa sababu Wilaya ya Hanang haina Gereza la Wilaya hivyo kulazimika
mahabusu kuhifadhiwa katika Gereza lililopo wilayani Babati. Akitolea ufafanuzi
hoja hiyo, Mhe. Kamuzora aliiahidi kulifikisha suala hilo kwa Viongozi husika
ili kuona namna bora ya kutatua changamoto hiyo.
Mhe.
Kamuzora alisisitiza mpangilio bora wa masijala, usafi wa mazingira ya Ofisi,
kuongeza uwajibikaji na ushirikiano katika utendaji kazi wa kila siku kwa ajili
ya kusaidia kufikisha malengo ya Mahakama.
Aidha,
ziara hiyo ya Ukaguzi pia ulihusiha ukaguzi wa maendeleo ya miradi ya ujenzi
ambayo imeanza hivi karibuni katika Mahakama za Wilaya ya Mbulu na Hanang na
kuwasisitiza Wakandarasi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kukamilisha ujenzi
huo ili majengo hayo yanze kutumika.
Wakati
leo tarehe 27 Machi, 2024 zoezi la ukaguzi limeendelea katika Gereza la Babati mjini
kwa ajili pia ya kusikiliza kero na maoni mbalimbali kutoka kwa wafungwa na mahabusu
wa Gereza hilo na kutolea ufafanuzi mambo mbalimbali yaliyohojiwa.
Ukaguzi
huo umeongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora,
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Manyara, Mhe. Bernard Mpepo, Msaidizi wa Sheria Mhe.
Thobias Kavishe, Mtendaji wa Mahakama Kuu Manyara, Bw. Jacob Swalle na Afisa
Tawala Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Bw. Christopher Msagati.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Endasak Wilayani Hanang. mara baada ya zoezi la ukaguzi. Wengine Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Manyara, Mhe. Bernard Mpepo (wa kwanza kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Mahakama.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Endagkot -Mbulu akisoma taarifa fupi ya Mahakama hiyo wakati wa zoezi la ukaguzi, kulia ni Msaidizi wa
Kumbukumbu wa Mahakama ya Mwanzo Endagkot Bw. Manswet Safari.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora akisikiliza taarifa ya utendaji kazi ya Mahakama ya Wilaya Mbulu iliyokuwa ikisomwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu
(Hayupo pichani).
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu Mhe. Johari Kijuwile
akisoma taarifa ya Mahakama ya Wilaya ya Mbulu wakati wa Ukaguzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni