Alhamisi, 28 Machi 2024

WADAU WA MASHAURI YA MADAI KIGOMA WAKUTANA KUWEKA MIKAKATI YA KUMALIZA MASHAURI

Na Aidan Robert, Mahakama Kuu-Kigoma

Wadau wa Mahakama katika mashauri ya Madai wameongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile jana tarehe 27 Machi, 2024 ili kujadili changamoto zilizopo na kuweka mikakati juu ya usikilizwaji wa mashauri yote ya madai yaliyosajiliwa katika Mahakama hiyo kwa usahihi na kwa haraka zaidi.

 

Akiongoza kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Rwizile aliitaka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutumia vema Sheria ya siku 90 za usuluhishi wa migogoro ya ardhi ili itatuliwe mapema kabla ya kufikishwa mahakamani na kupunguza wingi wa mashauri hayo dhidi ya Serikali.


“Ni muhimu kufanya hivi ili kuendana na kasi ya Mpango Mkakati wa Mahakama wa kutoa haki kwa wakati pamoja 
na kujiwekea mikakati imara ya umalizwaji wa mashauri ya madai,” alisema Jaji Mfawidhi.

 

Naye Wakili Mfawidhi Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mkoani Kigoma, Bw. Hemed Mkomwa aliipongeza Mahakama Kanda ya Kigoma kwa ushirikiano wanaoupata katika kusimamia mashauri ya Serikali.

 

 “Tunaipongeza Mahakama kwa ushirikiano mkubwa tunaoupata kwa kila hatua tunayofika katika usikilizwaji wa mashauri Mahakama Kuu,” alisema Bw. Mkomwa.

 

Ameahidi kutoa ushirikiano kwa Mahakama hasa katika kutumia Sheria ya siku 90 katika utatuzi wa migororo ya ardhi kabla ya kufikishwa mahakamani.

 

kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Mawakili wa Kujitegemea mkoani Kigoma, Bw. Eliutha Kivyiro aliishukuru na kuipongeza Mahakama kwa maboresho ya utendaji kazi kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwani Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashari (e-CMS) na ‘Judiciary portal’ umerahisisha upatikanaji wa namba za rejea “reference number” na usajili wa mashauri.

 

“Kwa Mawakili tunasajili mashauri bila kukwama kwa kuwa namba hizi zinapatikana kwa uharaka zaidi, hata hivyo tutashirikiana na Mahakama kutekeleza mikakati tuliyojiwekea ili kuwahisha usikilizwaji wa mashauri ya madai yaliyopo kwa ajili ya usikilizaji mahakamani,” alisema Bw. Kivyiro.

 

Wadau walioshiriki katika kikao hicho ni Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (SG), Jukwaa la Mawakili wa Kujitegemea, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya (DLHT).

 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, akisikiliza kwa makini taarifa iliyokuwa ikiwasilishwa na moja ya mjumbe wa Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma jana tarehe 27 Machi, 2024.

 


Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe.Francis Nkwabi akifuatilia Kikao cha Wadau wa Mashauri ya Madai wakati wa kutoa taarifa mbalimbali za wajumbe katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma jana tarehe 27 Machi, 2024.

 


Wakili kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Hemed Mkomwa akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa Kikao cha Wadau wa Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika  katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

 


Mwenyekiti wa Jukwaa la Mawakili wa Kujitegemea Mkoa wa Kigoma Bw. Eliutha Kivyiro akiwasilisha taarifa yake katika Kikao cha Wadau wa Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika  katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

 


Mjumbe kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bi. Fortunatha Muzee akifafanua jambo wakati wa kuwasilisha taarifa yake mbele ya wajumbe wa Kikao cha Wadau wa Kusukuma Mashauri ya Madai kilichofanyika  katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

 

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni