Na. Innocent Kansha-Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Wakandarasi na Wahandisi Washauri wa miradi ya ujenzi wa vituo sita Jumuishi vya Utoaji Haki (IJC) vinavyoendelea kujengwa nchini wasiwe kikwazo cha kukwamisha miradi hiyo kutokamilika kwa wakati na wanapaswa kuzingatia utekelezaji wa kandarasi zao kulingana na mikataba.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari mara baada ya kikao cha ndani na wakandarasi hao kilichofanyika Mahakama ya Rufani jijini Dar es salaam leo tarehe 6 Machi, 2024 Prof. Ole Gabriel amesema, mradi wa ujenzi wa vituo hivyo unagharimu fedha nyingi za walipa kodi, ni wajibu wenu kusimamia kazi hiyo kwa weledi wa kiwango cha hali ya juu na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora na muda wa mikataba ya ujenzi.
“Miradi
ya ujenzi wa vituo hivyo siyo tu unalenga kuongeza majengo ya Mahakama bali kushughulikia
jukumu muhimu la kuimarisha na kurahisisha mchakato wa utoaji haki kwa wananchi.
Ni vema kazi hiyo ikakamilika kwa wakati kwani wananchi wa maeneo husika
wanamatumaini makubwa na uaminifu kwa muhimili wa Mahakama”, amesisitiza Prof.
Ole Gabriel.
Prof
Ole Gabriel amesisitiza kuwa, lengo la mkutano huo na wakandarasi na wahandisi
washauri ni kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa miradi ya ujenzi wa IJC
inakamilika kwa wakati uliopangwa. “Tunatarajia wakandarasi na wahandisi
washauri kuweka kipaumbele na mkazo katika kukamilisha miradi hiyo kwa wakati
wa kimkataba,” ameongeza.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel, amesisitiza kwamba, Mahakama na Serikali
hazitavumilia sababu zozote za kizembe na zisizoendana na mikataba kwa mkandarasi
yoyote atakae fanya kazi katika ubora duni katika miradi hiyo.
Prof
Ole Gabriel ameonya kuwa Mahakama haitasita kusitisha kandarasi ya mkandarasi
yeyote na kumchukulia hatua za kisheria dhidi ya wakandarasi wasiotii sheria kwa
kushindwa kuzingatia mikataba yao halikadhalika kwa wahandisi washauri.
“Falsafa
ya sasa ya Serikali ni kutumia wakandarasi wa ndani yaani wazawa wenye uwezo na
hasa kwa kuzingatia na kutanguliza ubora na thamani ya matumizi ya fedha”, amesema
Prof. Ole Gabriel.
Mtendaji
Mkuu huyo amewaonya wakandarasi kutobweteka na kuridhika kwani muda wa
kimkataba haupo upande wao, akiwataka wahandisi washauri kudumisha viwango vya
ubora na kuhakikisha thamani ya pesa katika kila mradi.
Aidha,
Prof. Ole Gabriel ameongeza kuwa, ili kutatua changamoto za mara kwa mara za kiutendaji
katika kutekeleza miradi hiyo, amesisitiza kuwa ni umuhimu kudumisha
ushirikiano kati ya wakandarasi, wahandisi washauri na mahakama kwa kuimarisha
mawasiliano ya mara kwa mara.
Kisha
Mtendaji Mkuu, akawtaka Viongozi wa Serikali za Mitaa na Wabunge katika maeneo
yanayotekeleza miradi hiyo kuhamasisha wananchi kuthamini miradi hiyo huku
akisisitiza wajibu wao katika kuboresha upatikanaji wa haki.
Awamu
ya pili ya mradi wa ujenzi wa IJC unalenga kujenga vituo tisa, ambavyo
vinakadiriwa kugharimu takribani Shilingi bilioni 49.13 kwa miradi sita
inayoendelea kwa sasa. Awamu ya kwanza, iliyojumuisha miradi sita iliyokamilika
na kuanza kutumika, iligharimu Shilingi bilioni 51.45 amesema Prof. Ole
Gabriel.
Prof.
Ole Gabriel, amebainisha kuwa, Mahakama inajenga IJC ndogo yenye eneo la mita
za mraba 3,653, kwa gharama ya shilingi bilioni 7.2 na IJC kamili yenye eneo la
mita za mraba 5,300, iliyogharimu shilingi bilioni10.5. Miradi yote miwili
inafadhiliwa kupitia mkopo wa Benki ya Dunia.
Kati
ya miradi sita ya awamu ya pili, mmoja ni mradi wa IJC kamili unaojengwa mkoani
Songea. Miradi mingine mitano ya mikoa ya Simiyu, Njombe, Geita, Katavi, na
Songwe ni ya IJC ndogo.
Prof.
Ole Gabriel akabainisha kwamba, upimaji upya ‘remeasurement’ utafanywa kila mradi utakapokamilika ili
kuthibitisha usahihi wa malipo ya kifedha kwa kila mradi husika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni