Na Francisca Swai – Mahakama Musoma.
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, wameaswa kufanya kazi kwa heshima, upendo, umoja na kwa kuzingatia utu wa mtu kabla ya kuangalia wadhifa wake.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Kamazima Idd, aliwaasa watumishi hao, katika kikao cha makabidhiano ya ofisi kati ya Bw. Festo Chonya Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma anayehama na Bw. Leonard Maufi Mtendaji anayehamia Kanda ya Musoma, yaliyofanyika Machi 5,2024.
“Watumishi wote tufanye kazi kwa heshima, upendo, umoja, ushirikiano, kwa kujali utu wa mtu,kabla ya kuangalia wadhifa wake na siku zote tuzingatie njia ya mazungumzo kama sehemu nzuri ya kufikia muafaka katika mambo mbalimbali kama alivyokuwa akifanya Bw. Chonya.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya alimpongeza Bw. Festo Chonya kwa kazi nzuri aliyoifanya Musoma ya kutekeleza majukumu yake kwa misingi ya haki na kuunganisha watumishi kufanya kazi kwa umoja jambo lililochangia kwa Mahakama hiyo kuwa ya pili kitaifa kwa kasi nzuri ya umalizaji wa mashauri.
Kwa upande wake Bw. Festo Chonya, Mtendaji anayehama Kanda ya Musoma, aliwashukuru viongozi, watumishi na wadau wa Kanda hiyo kwa upendo na ushirikiano mkubwa waliompa wakati wote alipokuwa Musoma. Pia aliwaasa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa misingi uadilifu, weledi na uwajibikaji.
Aidha, Mtendaji mpya wa Kanda ya Musoma Bw. Leonard Maufi, aliwashukuru viongozi na watumishi kwa mapokezi mazuri na kuwaomba ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya kila siku ili kuweza kufikia malengo yanayotarajiwa na Mahakama ya Tanzania.
Watumishi wote kwa pamoja waliohudhuria kikao hicho cha makabidhiano kilichohudhuriwa na viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma na watumishi wa Mahakama Kuu Musoma na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma walikubaliana kuendelea kufanya kazi kwa upendo, umoja na ushirikiano ili kuhakikisha lengo kuu la utoaji haki sawa kwa wote na kwa wakati linafikiwa kama inavyotarajiwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (wa kwanza kulia), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Kamazima Idd (wa kwanza kushoto) wakishuhudia makabidhiano ya ofisi katika ya Mtendaji anayehamia Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi (wa pili kushoto) na Mtendaji anayehama Bw. Festo Chonya (wa pili kulia). Mtendaji anayehamia Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi (aliyesimama) akizungumza na viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma katika kikao cha makabidhiano ya Ofisi ya Mtendaji Kanda ya Musoma. Sehemu ya watumishi waliohudhuria kikao cha makabidhiano ya Ofisi ya Mtendaji Kanda ya Musoma wakifurahia jambo kwa pamoja wakati Afisa TEHAMA wa Kanda hiyo Bw. Simon Lyova (aliyesimama) akitoa neno la kwaheri kwa Bw. Festo Chonya na kumkaribisha Bw. Leonard Maufi. Mtendaji aliyehama Mahakama Kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya (katikati) akikata keki kwa furaha na Manaibu Wasajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha (wa kwanza kulia) na Mhe. Monica Ndyekobora (wa kwanza kushoto) wakati wa hafla fupi ya kumuga Mtendaji huyo. Mtendaji aliyehama Mahakama Kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Tawala, Maafisa Utumishi, Wahasibu, Afisa TEHAMA, Mkaguzi wa Ndani na Msimamizi wa Masjala wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma wakati wa hafla fupi ya kumuga Mtendaji huyo. Mtendaji aliyehama Mahakama Kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya (katikati) akipokea zawadi kutoka kwa watumishi wa Mahakama ya Wilaya Bunda ikionesha namna upendo wake ulivyofanya mahali pa kazi kuwa kama nyumbani, (kulia) ni Hakimu Mkazi, Mhe. Husna Msangi na (kushoto) Dereva wa Bunda Bw. Abriel Ezekiel. Mtendaji aliyehama Mahakama Kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya akitoa neno la shukrani na kwaheri kwa watumishi na wadau wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma (hawa kopichani) waliohudhuria katika hafla fupi ya kumuaga baada ya kupata uhamisho.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Mhe. Fahamu Mtulya (katikati), Mhe. Marlin Komba (kulia) na Mhe. Kamazima Idd (kushoto) kwa furaha wakitoa neno la shukrani kwa namna walivyofanya kazi na Mtendaji anayehama Bw. Festo Chonya pia kumtakia kila la heri katika kituo chake kipya. Mtendaji aliyehama Mahakama Kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya (wa kwanza kushoto) akipokea moja ya zawadi kutoka kwa watumishi wa Mahakama Kuu Musoma, ikiwa ni ishara ya ukumbusho wa Mbuga ya Serengeti inayopatikana Mkoa wa Mara, kama ishara ya kiongozi mahiri na shupavu pia kama zawadi kwake kutokana na mapenzi yake juu ya timu ya mpira ya Simba. Anayetolea maelezo ya zawadi hiyo ni Bw. Simon Lyova (kulia).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni