Jumatatu, 29 Aprili 2024

BARAZA JIPYA LA WAFANYAKAZI MAHAKAMA KUU KANDA YA GEITA LAKUTANA

  • Naibu Msajili mpya akaribishwa

Na Mwandishi Wetu-Mahakama, Geita

Kikao cha kwanza cha Baraza jipya la Wafanyakazi la Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita kimefanyika kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji.

Kikao hicho kiliendeshwa na Kaimu Mwenyekiti ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Griffin Mwakapeje kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina ambaye alikuwa kwenye majukumu mengine.

Aidha, ulifanyika uchaguzi wa Viongozi mbalimbali katika kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Mahakama wa Wazi katika jengo la Mahakama Kuu,.

Viongozi waliochaguliwa ni Katibu, Katibu Msaidizi pamoja na Mwakilishi wa Wajumbe wa Baraza hilo ambaye atakuwa anashiriki kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Taifa. 

Waratibu wa Uchaguzi huo walikuwa Bw. Mohamed Majaliwa ambaye ni Afisa Kazi Mfawidhi kutoka Ofisi ya Idara ya Kazi Mkoa wa Geita, akisaidiana na Bw. Emmanuel Zongwe, ambaye ni Katibu TUGHE Mkoa wa Geita.

Matokeo ya uchaguzi huo uliokuwa na jumla ya wajumbe 28, yanaonesha kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Nyang’hwale, Mhe Idran Chuvaka alichaguliwa kuwa Katibu wa Baraza la Wafanyazi,.

 Afisa Utumishi Mahakama Kuu Geita, Bi. Happiness Mushi alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi na Mlinzi Mwandamizi Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Bw. Dotto Marando alichaguliwa kuwa Mjumbe atakayewakilisha kwenye Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama.

Kadhalika, wajumbe wa Baraza walipokea na kujadili taarifa mbalimbali, ikiwemo na hoja za wafanyakazi zilizoibuliwa katika mwaka uliopita (2022/2023) kama zimeshajibiwa kwa kupatiwa ufumbuzi.

Kikao kiliazimia msisitizo zaidi wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)katika uendeshaji wa shughuli zote za Mahakama kwani Geita ni Mkoa ambao uliteuliwa kuwa wa mfano katika matumizi hayo.

Wakati huo huo, Mahakama Kuu Kanda ya Geita hivi karibuni ilifanya hafla fupi ya kumkaribisha Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala ya Geita, Mhe. Fredrick Lukuna aliyehamishiwa katika Kanda hiyo akitolea Arusha. 

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Watumishi mbalimbali, wakiwemo Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mkoa na Wilaya za Geita, Chato, Bukombe, Nyang’hwale na Mbogwe. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mwakapeje alihimiza Watumishi kuendeleza ushirikiano, umoja na upendo kwa wote na kushiriki kwenye matukio yanayowakutanisha na kufurahi kwa pamoja.

Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Griffin Mwakapeje (katikati aliyesimama) akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Geita, Bi. Masalu Kisasila.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Geita (juu na picha mili chini) wakifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajiri wakati wa kikao hicho.


Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Griffin Mwakapeje (katikati aliyesimama) akizungumza katika hafla ya kumkaribisha Naibu Msajili, Mhe.Fredrick Lukuna. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Geita, Bi. Masalu Kisasila.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Geita (juu na picha mili chini) wakifuatilia mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajiri katika hafla hiyo.



(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni