Alhamisi, 25 Aprili 2024

JAJI KIONGOZI: TEHAMA IMEPUNGUZA MUDA WA SHAURI KUKAA MAHAKAMANI NA MLUNDIKANO

 Na Magreth Kinabo-Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mchakato wa usikilizaji wa mashauri, yamesaidia kupunguza muda wa shauri kuwa mahakamani na mlundikano wa mashauri, hivyo ni hatua ambayo Mahakama inapaswa kujivunia

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 25 Aprili, 2024 na Mhe. Siyani wakati akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha tatu cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu katika ukumbi wa hoteli ya Alexander mjini Iringa.

Mwaka 2023, kwa mfano; Mahakama ilikuwa na mlundikano wa asilimia nne (4), hata hivyo kufikia mwezi Machi, 2024 mlundikano wa mashauri umepungua hadi kufikia asilimia tatu (3). TEHAMA pia imewezesha muda wa kumaliza mashauri unaopimwa kila mwisho wa mwaka kupungua. 

Kwa mfano mwaka 2023 mahakama ilitumia wastani wa siku themanini na nne (84) kukamilisha usikilizwaji na utoaji wa maamuzi kwa shauri, ukilinganisha na siku 95 kwa mwaka 2022. Haya ni mafanikio makubwa tunayopaswa kujivunia,” amesema Jaji Kiongozi

Aidha Mhe. Jaji Siyani kupitia baraza hiloamesisitiza juu ya umuhimu wa watumishi wote kukumbuka malengo tuliyojiwekea kama taasisi katika kutoa huduma kwa wananchi sambamba na kufahamu mipango ya kufanikisha malengo hayo ili kuwezesha kila mmoja kushiriki kikamilifu kutekeleza mipango hiyo. Malengo makuu yameainishwa katika mpango Mkakati wa Mahakama tunaoutekeleza sasa ambayo ni kupunguza muda wa mashauri kuwa Mahakamani na kuongeza imani kwa wananchi kwa kutoa huduma bora kwa wakati. 

Kwa hiyo kila mmoja wetu anao wajibu wa kuhakikisha malengo hayo yanatimia katika viwango stahiki. Ni vyema watumishi wa mahakama wakafahamu vigezo vinavyotumika kupima ufanisi wetu wa kazi  ili kila mmoja aweze kujua jinsi ya kuchangia katika vipimo hivyo na hii itatutoa katika utendaji kazi kwa mazoea na hivyo kutekeleza majukumu yetu kimkakati. Hili ni muhimu kwa sababu, jukumu la kuhakikisha lengo la kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati linafikiwa, ni la kila mmoja wetu,amesisitiza.

Akizungumzia kuhusu Baraza hilo la wafanyakazi, amesema ni fursa ya kisheria kwa watumishi kujadiliana na menejimenti ya taasisi yao juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja; na maslahi yao kama watumishi kwa upande mwingine. Kwa hiyo; mabaraza haya ni chombo cha ya kusikiliza changamoto za wafanyakazi lakini ni mashine ya kuchakata changamoto hizo kwa lengo la kuimarisha mazingira ya kazi kwa faida ya pande zote mbili. 

Mhe. Jaji Siyani amewakumbusha umuhimu wa kufanya kazi kwa uadilifu na uweledi. Huku akisema mambo haya mawili ni kama ibada, hatuwezi kuacha kukumbushana kila tunapokutana

Nitumie fursa hii kuwapongeza watumishi wote wa mahakama kote nchini wanaoendelea kuchapa kazi kwa juhudi, uadilifu, akili na weledi licha ya changamoto zilizopo. Ninatambua yapo matukio machache yanayoashiria ukosefu wa maadili. Niwahakikishie uongozi wa Mahakama utaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo hivyo ili kulinda hadhi ya mhimili wetu na kujenga imani ya wananchi kwa taasisi hii,” amesema

Aliwataka watumishi hao kujenga umoja, amani na mshikamano miongoni mwaoKwa kuwa mambo haya matatu ni muhimu na ya msingi kwa mendeleo ya taasisi yoyote.Hivyo ni lazima sote tuepuke majungu na mambo yanayoweza kuharibu mahusiano yetu. Badala ya watu kupiga ubuyu kazini, ni bora wapige kazi. 

Jaji Kiongozi huyo amefafanua kuwa mahusiano kazini yanaweza kujengwa kwa njia nyingi. Moja wapo ni ushiriki wa michezo na uanzishwaji wa vikundi vya mazoezi, hivyo  kupitia baraza hilaliwaomba viongozi wa mahakama kote nchini, kuanzisha utaratibu wa mazoezi kazini pamoja na michezo katika muda ambao hautaathiri majukumu ya kazi.

Amewasihi wajumbe wa baraza hilo kuwa wa kwanza kubadilika kutokana na elimu watakayojifunza, kisha waifikishe wenzao waliobaki vituoni, ili nao iwasaidie kubadilika na hatimaye mabadiliko hayo yaongeze tija katika utekelezaji wa kazi zao.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akisisitiza jambo wakati akiongea na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Mahakama Kuu - Masjala Kuu.

  Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu) wakifuatilia mjadala wakati wa kikao hicho.

 Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu) (juu na picha mbili chini) wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (mwenye miwani aliyekaa katikati)


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni