Alhamisi, 25 Aprili 2024

WATUMISHI WA MAHAKAMA WASISITIZWA KUWA WAADILIFU, WELEDI

Na Lusako Mwang’onda-Mahakama, Iringa

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wametakiwa kufanya kazi kwa ueledi na uadilifu wa hali ya juu wakiwa katika majukumu yao ya kuwatumikia wananchi. 

Hayo yamesemwa leo tarehe 25 Aprili, 2024 na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustafa Mohamed Siyani wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu (Masjala Kuu) kilichofanyika mjini hapa katika Hoteli ya Mount Royal Villa. 

Mhe. Siyani amesema si vyema kwa mtumishi wa Mahakama kuwa na uadilifu unaotiliwa shaka maana hali hiyo hushusha Imani ya wananchi kwa Mahakama.

Jaji Kiongozi, ambaye kikanuni ndiyo Mwenyekiti wa Kikao hicho amesema, “imani ya wananchi ni kubwa sana kwa Mahakama, hivyo uongozi wa Mahakama hautamfumbia macho mtu yeyote ambaye kwa namna yeyote ile atataka kuitia doa Imani waliyonayo wananchi kwa muhimili huu”.

Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi ambacho kikanuni kinakuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Kiongozi kimehudhuriwa pia na Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu) na kwa upande mwingine viongozi na wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi yaani TUGHE nao walikuwepo kuwasilisha hoja za Wafanyakazi.

Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi kimetoka na maazimio mbalimbali, ikiwemo Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuendelea kupewa kipaumbele katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kimahakama. 

Naye mwenyekiti wa kikao hicho, amesisitiza kuwa kufanya kazi kwa weledi katika zama hizi ni lazima kuendane na matumizi ya TEHAMA. 


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustafa Mohamed Siyani akisisitiza jambo wakati akiongea na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Mahakama Kuu - Masjala Kuu.

Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu) wakifuatilia mjadala wakati wa kikao hicho.

Mtendaji wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania (MMK), Bw.Leonard Magacha akifuatilia kwa makini mijadala mbalimbali wakati wa kikao hicho cha Baraza.

Makundi mbambali ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu) (juu na chini) wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustafa Mohamed Siyani (mwenye miwani aliyekaa katikati).

Makundi mengine ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu) (juu na picha mbili chini) wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustafa Mohamed Siyani (mwenye miwani aliyekaa katikati).


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni