Alhamisi, 25 Aprili 2024

VIONGOZI WA TUGHE MKOANI SINGIDA WAIPONGEZA MAHAKAMA KWA KUWAJALI WATUMISHI

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) wameipongeza Mahakama Kanda ya Dodoma kwa kuwajali watumishi ikiwa ni pamoja na kuzingatia maslahi yao.

Pongezi hizo zilitolewa na Viongozi hao waliohudhuria katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Dodoma lililofanyika jana tarehe 24 Aprili, 2024 mkoani Singida.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Singida, Dkt. Athuman Bunto alisema, “naipongeza sana Mahakama kwa kuzingatia na kufuata Sheria za utumishi kwani wamezingatia maslahi ya watumishi, sehemu kubwa ya bajeti inawagusa watumishi, mafunzo kutolewa katika Kada zote kwa ajili ya kujengeana uwezo, hiki ni kitu kizuri.” 

Aidha, amelisifu Baraza hilo kuwa, limeendeshwa kwa uwazi watumishi wameonekana kuridhika na limekuwa shirikishi kwani hoja zilizotolewa zilipatiwa majibu na kwa zile ambazo zilikuwa chini ya uwezo wa Kanda wajumbe wamekubaliana kuziwasilisha katika Baraza Kuu.

Kikao hicho kiliongozwa na Mhe Jaji Mfawidhi  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo.


Katika Baraza hilo, taarifa za bajeti zilisomwa kutoka Mikoa yote Miwili ya Singida na Dodoma na kuona utekelezaji wake hususani kwenye maeneo yanayowahusu watumishi moja kwa moja na pia kuona vipaumbele vya bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Akihitimisha kikao cha Baraza hilo, Mhe. Dkt. Masabo aliwasisitiza watumishi kuendelea kuwaelekeza na kuwasaidia wateja wanaofika mahakamani kuhusiana na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA na Mifumo mbalimbali ya Mahakama kwa kuwatia moyo na kuona mabadiliko ya TEHAMA ni msaada kwao. 

Vilevile, aliwataka wajumbe wa Baraza kuzingatia azimio la Morogoro kuhusu utunzaji wa Mazingira kwa kuendelea kutunza mazingira na kupanda miti ya vivuli na matunda.



Viongozi wa Baraza la wafanyakazi Kanda ya Dodoma wakifurahia jambo katika kikao cha Baraza la Kanda hiyo kilichofanyika tarehe 24 Aprili, 2024, aliyeketi mbele (katikati) ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo, Mhe. Dkt. Juliana Masabo. Wa kwanza kushoto ni Katibu wa TUGHE Mkoa wa Singida, Bw.Shedrack anayemfuatia ni Bw. Gerald Gamba, Katibu wa Baraza hilo na walioketi mbele, wa kwanza kushoto ni Katibu Msaidizi wa Baraza, Bi Dorice Busanji akifuatiwa na Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Singida, Dkt. Athumani Bunto.


Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Kasuka akichangia jambo katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mahakama Kanda ya Dodoma.

Sehemu ya wajumbe waliohudhuria Baraza hilo kutoka Wilaya za Dodoma.

Sehemu ya wajumbe kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma waliohudhuria Baraza hilo mkoani Singida.


Sehemu ya wajumbe kutoka Mahakama za Wilaya Singida waliohudhuria kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Dodoma.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni