Jumatano, 24 Aprili 2024

MAHAKAMA SPORTS YANG’ARA MASHINDANO YA MEI MOSI 2024

Na Seth Kazimoto - Mahakama Kuu Arusha

 

Timu ya Mahakama Sports imeshinda mechi zake zote ilizocheza mpaka sasa katika mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea katika viwanja vya Ngarenaro jijini Arusha baina ya Taasisi mbalimbali za Serikali.

 

Mahakama inashiriki mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume ambapo Timu ya Wanawake ipo katika kundi D lenye Timu za Wizara ya Mambo ya Ndani, Mahakama, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Arusha Jiji na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania.

 

Timu ya Kuvuta Kamba Wanaume ipo katika kundi A pamoja na timu za Wizara ya Maliasili, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wizara ya Mawasiliano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

 

Mpaka sasa, Timu ya Kuvuta Kamba Wanawake imecheza mechi tatu na kushinda zote. Katika mechi hizo, Mahakama ilizichapa bila huruma Timu za Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), Arusha Jiji na Wizara ya Mambo ya Ndani.

 

Vilevile, Timu ya Wanaume mpaka kufikia tarehe 19 Aprili, 2024 ilikuwa tayari imecheza mechi mbili na kushinda zote, katika mechi hizo, Mahakama ilizikung’uta Timu za Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

 

Aidha, Uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ukiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. JoachimTiganga, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Mariam Mchomba na Mtendaji wa Mahakama Kuu Arusha, Bw. Festo Chonya, ulikutana na Timu ya Mahakama katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha na kuipongeza timu kwa umahiri wake na kuwatia moyo kuendeleza ushindi kwa mechi zote zilizobaki. 

 

Timu ya Mahakama inanolewa na Kocha mahiri, Bw. Spear Dunia Mbwembwe na imeambatana na Viongozi wa Timu hiyo wakiwemo Naibu Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Bw. Fidelis Choka, Afisa Michezo wa Mahakama, Bw. Peter Machalo na Katibu wa Mahakama Sports, Bw. Donald Tende. 

 

Mashindano hayo baina ya wafanyakazi wa Umma yanalenga kudumisha umoja, mshikamano na kuimarisha afya. Taasisi mbalimbali zinashiriki mashindano hayo ambazo ni pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Ununuzi wa Umma Tanzania (PPRA), Ikulu, Wizara ya Mipango, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Wizara ya Maji.

 

Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi kitaifa mwaka huu yanatarajiwa kufanyika mkoani Arusha huku maandalizi ya awali yakifanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha akiwapongeza na kuwatia moyo wachezaji wa Timu ya Mahakama Sports katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 19 Aprili, 2024.


 


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Mariam Mchomba akiwa na wachezaji wa Mahakama Sports katika ukumbi wa mikutano (IJC) Arusha tarehe 19 Aprili, 2024 alipokutana nao kwa lengo la kuwapongeza na kuwatia moyo.



Kocha wa Mahakama Sports, Bw. Spear Dunia Mbwembwe.


Timu ya Mahakama Sports ikiwa mazoezini katika viwanja vya Ngarenaro Jijini Arusha wakiongozwa na kocha wa tumu (anayeonekana mbele) Bw. Spear Dunia Mbwembwe.



Wachezaji wa Mahakama Sports wakiwa katika picha ya pamoja.


Timu ya Wanawake ya Kuvuta Kamba ya Mahakama (upande wa kushoto) wakiwavuta kwa ujasiri Timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani (upande wa kulia) tarehe 19 Aprili, 2024 katika viwanja vya Ngarenaro Arusha. Timu ya Mahakama iliishinda Timu ya Wizara ya Mambo ya ndani mivuto 2 kwa nunge (0).



Timu ya Mahakama Sports ikishangilia ushindi baada ya kuishinda timu ya Wizara ya Mambo ya ndani mivuto miwili kwa sifuri.

 

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni