Jumanne, 23 Aprili 2024

JAJI KIHWELO AHIMIZA UWELEDI, UADILIFU KATIKA KUKABILI UHALIFU DHIDI YA WANYAMAPORI

NA MWANDISHI WETU

Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amesema kuwa uweledi na uadilifu unahitajika zaidi katika kushughulikia mashauri ya uhalifu dhidi ya wanyamapori ukiwemo ujangili na makosa ya misitu kwa sababu mashauri hayo yana changamoto kubwa katika kuyaendesha, ikizingatiwa kuwa uhalifu huo unavuka mipaka.

Jaji Kihwelo amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya kundi la nne yanayohusu namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori ukiwemo ujangili na makosa yanayohusiana kwa wadau wa haki jinai zaidi ya 60  tarehe 22/04/2024 hapa Chuoni Lushoto.

Mafunzo hayo yatakayochukuwa wiki mbili mpaka tarehe 03/05/2024 yanaendeshwa na IJA kwa ufadhili wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya PAMS Foundation inayojihusisha na uhifadhi wa mazingira na usalama wa Wanyamapori na washiriki ni Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu, Waendesha Mashtaka   na Wapelelezi wa vyombo mbalimbali vya Serikali wakiwemo TAWA, TANAPA, TFS, NCCA , kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Kilimanjaro na Tanga. 

 “Mashauri ya makosa dhidi ya Ujangili na misitu yana changamoto kubwa sana, kwa sababu haya makosa yanagusa uchumi wa taifa, nani makosa ya kimataifa,hivyo ili watu waweze kuamua mashauri hayo kwa wakati na inavyostahili, ni vema wawe na uelewa wa kutosha, na matarajio yetu baada ya mafunzo haya kutakuwa na uboreshaji mkubwa katika kukabiliana na makosa haya,” amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.

Pia, Mhe. Jaji Kihwelo amewapa wito maafisa wote wanaoshiriki mafunzo hayo na wengineo kushughulikia mashauri ya uhalifu dhidi ya Wanyamapori kwa uweledi na uadilifu pamoja na kuongozwa na dhamira zaidi.

Kwa Upande wake, Samson Kasaala ambaye ni Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni wa PAMS Foundation, amebainisha kuwa taasisi yake imefadhili mafunzo haya ili kuhakikisha wadau hao wanaboresha uweledi  katika utendaji wao wa kazi na hivyo kukabiliana ipasavyo na uhalifu huo wa wanyamapori.

Pia ameongeza: “Niwaombe wadau hao wawe na uweledi na kutenda haki, kuhakikisha kesi zote zinasikilizwa kwa haki na hukumu zinakuwa za haki, kwa sababu wao wana wajibu wakulinda mali zetu ambazo ni sehemu muhimu ya uchumi kama utalii.”

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Majaji wa Mahakama Kuu, Waendesha Mashita kutoka Ofisi ya Mashtaka ya Taifa, Maafisa kutoka Jeshi la Polisi na Mamlaka mbalimbali zinazojihusisha na upelelezi pamoja na uhifadhi wa Maliasili.

Nao baadhi ya washiriki wa Mafunzo hayo akiwemo Afisa Uhifadhi wa Wanyama Pori kutokea Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA)Kanda ya Arusha Matika Chacha amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia katika kuboresha masuala ya upelelezi na hivyo kupatikana kwa ushahidi mzuri utakaowezesha kuwajibishwa kwa wahusika wa uhalifu dhidi ya Wanyamapori na makosa ya misitu.

Kwa upande wake Afisa Misitu kutokea wakala wa huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Kaskazini Zayana Mrisho amesema kuwa mafunzo hayo yatawasadia kupata uelewa mpana juu ya taratibu bora za ukamataji wa wahalifu na kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani bila kuathiri mwenendo mzima wa tukio zima.

Aidha, makundi matatu ya mafunzo haya yamekwishafanyika katika mikoa ya Morogoro, Katavi na Iringa huku awamu ya tano ikitarajiwa kufanyika wilayani Tarime mkoani Mara mwezi Mei mwaka huuu ambapo mpaka kumalizika kwa mafunzo, jumla ya washiriki 785 watakuwa wamepatiwa mafunzo hayo.

Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akihutubia na kufungua mafunzo ya yanayohusu namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori na misitu Chuoni Lushoto mkoani Tanga.

3. 

Mratibu wa mafunzo Endelevu ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Hakimu Mkazi, Mhe. Husna Rweikiza akitoa neno la utangulizi wakati wa Mafunzo  yanayohusu namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori na misitu yanayofanyika  Chuoni Lushoto mkoani Tanga.

Baadhi ya washiriki wa Mafunzo  yanayohusu namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori na misitu yanayofanyika  Chuoni Lushoto mkoani Tanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Mteule akitoa neno la ukaribisho wakati wa Mafunzo  yanayohusu namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori na misitu yanayofanyika  Chuoni Lushoto mkoani Tanga.

Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Washiriki ambao ni Majaji wa Mahakama Kuu wakati wa Mafunzo  yanayohusu namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori na misitu Chuoni Lushoto mkoani Tanga. Kushoto  ni Jaji wa Mahakama Kuu (T) kanda ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi, anayefuata ni Mhe. Salma Maghimbi, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu(T) kanda ya Dar es Salaam, na wa mwisho ni Jaji wa Mahakama Kuu (T), kanda ya Manyara, Mhe.Setephen Magoiga.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni