Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma
Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wapo mkoani Kigoma katika kikao cha kusikiliza jumla ya mashauri 26 yaliyopangwa katika kikao hicho kilichoanza jana tarehe 22 Aprili, 2024 kwenye jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Flora Mtarania alisema jopo la Majaji hao limejipanga imara kusikiliza Jumla ya Mashauri 26, ambapo kati ya mashauri hayo 13 ni rufaa za jinai, sita ni rufaa za Madai, pamoja na maombi ya madai saba.
“Jopo hilo la Majaji litasikiliza mashauri kwa muda wa majuma matatu kwa takribani siku 21 mfululizo,” alisema Mhe. Mtarania.
Aidha alisema, jopo hilo la Majaji wa Rufani wanakusudia kusikiliza mashauri matatu kwa siku yaani kuanzia jana tarehe 22 Aprili, 2024 hadi tarehe 10 Mei, 2024, ambapo wanatarajia kuhitimisha kikao hicho.
Ameongeza kuwa, wamepanga kusoma Hukumu au maamuzi ya kikao hicho kwa mujibu wa ratiba hiyo ili kuendana na Mpango Mkakati wa Mahakama.
Majaji wa Mahakama ya Rufani waliopo katika vikao hivyo ni Mhe. Mwanaisha A. Kwariko ambaye ni Mwenyekiti wa jopo hilo wengine ni Mhe. Zephrine Galeba na Mhe. Dkt. Benhaji Masoud.
Mapema kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile aliwaongoza watumishi wa Kanda hiyo kuwapokea Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani waliofika kwa ajili ya kuanza vikao vya Mahakama ya Rufani vilivyopangwa kufanyika katika Kanda hiyo.
Picha ya pamoja ya Wasaidizi wa Sheria wa Majaji wa Mahakama ya Rufani (katikati) ni Mhe. Khalfan Khalfan, kulia ni Mhe. Julieth Musiza na kushoto ni Mhe. Dorothy Mateni wakiwa katika maandalizi ya kuanza kikao cha Mahakama ya Rufani kilichoanza katika Kanda hiyo jana tarehe 22 Aprili, 2024.
(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni