Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile hivi karibuni alifanya ziara kikazi ya Mahakama na Magereza katika Wilaya ya Kibondo na kusisitiza, pamoja na mambo mengine, matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani.
Akiwa katika Gereza la Nyamisivyi Kibondo, Mhe. Rwizile aliambatana na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kigoma, Mhe Gadiel Mariki, Mtendaji wa Mahakama Kigoma, Bw. Benjamin Mlimbila na Afisa TEHAMA wa Mahakama, Bw. Prosper Bonaventura.
Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa kati ya mifumo ya TEHAMA iliyojengwa na Mahakama, Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) ndio mama ambao unahusika katika kusajili na kuratibu usikilizaji wa mashauri. Aliongeza kuwa utoaji haki utaharakishwa kama Wadau watashirikiana na Mahakama katika matumizi ya mfumo huo.
“Tunapaswa kushirikiana wote ili kuharakisha usikilizwaji wa mashauri, rufaa zote zinapaswa kusajiliwa mara tu hukumu inapotoka pale mhusika anapokuwa na nia ya kukata rufaa. Kwa sasa hatutegemei kupokea malalamiko ya nakala za hukumu maana siku hukumu inaposomwa ndio nakala inapaswa kutoka na wahusika wa mashauri wanapaswa kupewa siku hiyo,” alisema.
Jaji Mfawidhi alieleza pia kuwa lengo la kuambatana na Afisa TEHAMA katika ziara hiyo ni kuhakikisha Maafisa wa Magereza wanapata elimu ya utumiaji wa mifumo ya TEHAMA iliyopo mahakamani na pia Wafungwa na Mahabusu waweze kupata uelewa wa kutosha.
Alisisitiza kuwa Mahakama Kuu Kigoma inakusudia kusikiliza kwa mfululizo mashauri yote yenye umri unaozidi miezi sita. Mhe. Rwizile alibainisha kuwa wanampango wa kuwatumia Mahakimu wenye mamlaka ya nyongeza ili kuharakisha usikilizwaji wa mashauri hayo na kutoa haki kwa wakati.
Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, aliuhimiza uongozi wa Magereza katika Wilaya hiyo kusimamia matumizi ya mifumo ya TEHAMA iliyopo mahakamani ili kuwasaidia Wafungwa wenye nia ya kukata rufaa zao.
Alisema kuwa mifumo iliyopo inaruhusu kufungua rufaa kwa mtu akiwa gerezani. Mhe. Mariki alieleza pia manufaa ya TEHAMA kuwa Wafungwa wanapata nakala zao kwenye mfumo mara baada ya hukumu kusomwa.
Naye Mkuu wa Gereza la Nyamisivyi Kibondo, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Peter Shaban alimshukulu Jaji Mfawidhi na ujumbe wake kwa kufanya ziara hiyo pamoja na kuzungumza na Wafungwa na Mahabusu. Aliahidi kuzifanyia kazi changamoto ambazo zipo katika mamlaka yake, hasa kusimamia ufunguaji na usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya TEHAMA.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Gereza la Kibondo Nyamisivyi Peter Shaban (kushoto), akifuatiwa na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Kigoma, Bw. Benjamin Mlimbila na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kibondo, Mhe. Maila Makonya.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni