Ijumaa, 5 Aprili 2024

MATUNDA YA MUUNGANO YAJIDHIHIRISHA MAHAKAMANI


Na Magreth Kinabo -Mahakama

 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kumekuwapo na ongezeko la asilimia 100 la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 5 Aprili, 2024 kwenye mkutano ulioandaliwa na Idara ya Habari (Maelezo) kwenye ukumbi wa jengo la PSSSF Jijini Dodoma, Prof. Ole Gabriel amesema ongezeko hilo la Majaji limeenda sambamba na uanzishwaji wa  Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani nchini. 

 

“Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiingia madarakani Machi 2021, kulikuwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania 16, na katika uongozi wake hadi kufikia tarehe 03 Septemba, 2023 idadi imeongezeka na kufikia 35, ikiwa ni zaidi ya asilimia 100,” alisema na kuongeza kuwa kati ya Majaji hao, 12 ni wanawake na 23 ni wanaume ambao watatu wanatoka Zanzibar.

 

Aidha, Mtendaji Mkuu ameeleza kwamba ongezeko hilo kwa sasa linawezesha majopo 11 ya Majaji watatu, majopo saba ya Majaji watano na majopo matano ya Majaji saba wakati wa kuendesha vikao vya Mahakama ya Rufani kwa wakati mmoja. 

 

 Ameongeza kwamba idadi ya vituo vya kusikilizia mashauri ya Mahakama ya Rufani imeongezeka na kutoka 16 wakati wa Mhe. Dkt. Samia akiingia madarakani na kufikia vituo 18 mpaka sasa.

 

Amevitaja vituo vya usikilizaji wa Mashauri ya Mahakama ya Rufani  viko katika Masjala za Mahakama Kuu za Arusha, Dar es Salaam, Bukoba, Dodoma, Iringa, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Moshi, Musoma, Mtwara, Mwanza, Shinyanga, Songea, Sumbawanga, Tabora, Tanga na Zanzibar.

 

Prof. Gabriel amezitaja faida zilizotokana na kuongezeka kwa Majaji wa Mahakama hiyo ambazo ni kupunguza mlundikano wa mashauri, kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi katika Masjala zote za Mahakama Kuu, Mashauri kusajiliwa na kuamuriwa kwa wakati na kupungua mzigo kwa majopo yaliyokuwepo.

 

Prof. Ole Gabriel ameeleza kuwa kumekuwepo na mahusiano mazuri kwa upande wa watumishi kati ya Mahakama upande wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa kipindi hicho cha muungano ambapo watumishi kutoka Zanzibar wamekuwa wakija Tanzania Bara na wale wa Tanzania Bara huenda Zanzibar ili kubadilishana uzoefu. 

 

 

“Tumekuwa na ushirikiano kati ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania Bara na Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Zanzibar. Hivyo nadhani imefika mahali Watanzania waelewe matunda ya muungano yameimarika,” alisisitiza.

 

Mtendaji huyo pia amesema ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki(IJC) Pemba, ambao utaanza hivi karibuni ni miongoni mwa mafanikio yanayolenga kusongeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi. Amesema kuwa uwepo wa Kituo hicho utaiwezesha Mahakama ya Rufani kuwa na Masjala yake ndogo na  kuongeza idadi ya Vikao vya Mahakama kwa upande wa Zanzibar.

 

 Mahakama ya Rufani ya Tanzania, ilianzishwa mwaka 1979 na Majaji wa  watano idadi hiyo ikimjumuisha Jaji Mkuu, wakifanya kazi  katika Masjala ya Dar es Salaam.

 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 5 Aprili, 2024 kwenye mkutano ulioandaliwa na Idara ya Habari (Maelezo) kwenye ukumbi wa jengo la PSSSF Jijini Dodoma, Prof. Ole Gabriel kuhusu miaka 60 ya muungano.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Bi. Zamaradi Kawawa akizungumza jambo kwenye mkutano huo.

 


                    Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo. 




Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati aliyekaa mbele)akiwa kwenye mkutano huo. Wengine ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mhe. Elimo Massawe ambaye amemwakilisha Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Utawala na  Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania,Bi.Beatrice Patrick (wa pili kushoto,)Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Bi. Zamaradi Kawawa(wa kwanza kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi Tathimini na Ufuatiliaji wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Sebastian Lacha.


Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Steven Magoha(watatu kushoto), Katibu wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Bw. Majuto Mdenya(wa pili kushoto),Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma cha Mahakama ya Tanzania,Bw. Gerard Chami na Maafisa Habari Wandamizi (wa pili kulia) ni Bi. Mary Gwera na (wa kwanza kulia)ni Bi.Magreth Kinabo.

                                         (Picha na Faustine Kapama - Mahakama)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni