Ijumaa, 5 Aprili 2024

KISHINDO CHA MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMANI KIKUBWA: MTENDAJI MKUU

Na Innocent Kansha- Mahakama, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kishindo cha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ndani ya Mahakama ya Tanzania ni kikubwa.


Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari leo tarehe 5 Aprili, 2024 kwenye Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Mahakama ya Tanzania ndani ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Prof. Ole Gabriel ametoe wito kwa Taasisi zingine za Umma kutumia mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.


“Kwenya teknolojia tuko vizuri sana, Mahakama ya Tanzania ni ya pili baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika matumizi ya TEHAMA,” amesema Mtendaji Mkuu.


Prof. Ole Gabriel amebainisha kuwa Mahakama imekuwa mstari wa mbele katika matumizi ya Ofisi mtandao ‘e-Office’ na katika eneo hilo wamefikia asilimia 99.9. “Sikumbuki ni lini mimi nimekaimisha Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama, kwanza ni aibu kipindi hiki cha teknolojia,” ameongeza Prof. Ole Gabriel.


Aidha, Mtendaji Mkuu alieleza kuwa Mahakama ya Tanzania imeanzisha mfumo wa akili bandia ambao unajulikana kwa jina jingine kama “akili mnemba” ili kuwarahisishia Majaji na Mahakimu wakati wa usikilizaji wa mashauri.


Mtendaji Mkuu ameongeza kuwa kwenye masuala ya usimamizi wa mashauri kwa kutumia mfumo mpya wa ‘e-CMS’ umeendelea kuboresha shughuli za utoaji haki, kwani mashauri yanasajiliwa kitijiti, yanapokelewa kidijiti, yanatolewa maamuzi kidijiti na kupandishwa kwenye mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya rejea na kumbukumbu.


“Mashauri hayo hupandishwa kwenye mtandao wa kidunia wa TanzLII ambao ni wa kwanza kidunia kutembelewa kwa asilimia 84.2, ukifuatiwa na Nchi fulani kubwa yenye asilimia 2.7,” amesema Mtendaji Mkuu. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari leo tarehe 5 Aprili, 2024 kwenye Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Mahakama ya Tanzania ndani ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Sehemu ya Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma wakifuatilia mkutano wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Mahakama ya Tanzania ndani ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Mkurugenzi Msaidizi Habari Maelezo Bi. Zamaradi Kawawa akifafanua jambo wakati wa mkutano huo.

Sehemu ya waandishi wa Habari walioshiriki mkutano huo.

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni