Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amewataka Wasajili wapya wa
Mahakama kuendeleza maboresho yanayofanywa ndani ya Mhimili wa Mahakama.
Akizungumza na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe.
Eva Kiaki Nkya na Msajili wa Mahakama Kuu Mhe. Chiganga Mashauri Tengwe mara
baada ya viongozi hao kuapishwa jana, Jaji Kiongozi alisema maboresho yote
yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania yanalenga kuboresha huduma ambazo Mahakama
inazitoa kwa Wananchi.
”Kwa nafasi mlizonazo sasa mna fursa nzuri zaidi ya
kuwatumikia watanzania kwa kuwa Wasajili ndiyo injini au Moyo wa Mahakama ya
Tanzania”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika
matumizi ya mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha utoaji wa huduma zake kwa
wananchi hivyo haitarajiwi viongozi hao kurudisha nyuma juhudi zilizofanyika.
Aliwataka kusimamia kikamilifu utendaji
kazi wa Mahakama zote nchini.
”Kufikia Mwaka 2025, Mahakama ya Tanzania itakuwa ikitoa
huduma zake zote kwa mtandao, na tayari safari hiyo imeshaanza hivyo ninyi
mnapaswa kuwa madereva wetu wazuri”, alisema Jaji Kiongozi.
Kuhusu ufanisi katika kazi zao, Mhe. Siyani aliwashauri
Viongozi hao wapya kuwa na utamaduni wa kujipima wenyewe utendaji kazi wao kwani
kujipima wao wenyewe ni vizuri kuliko kusubiri kukosolewa au kusikia malalamiko.
Awali akizungumza wakati wa hafla ya kuapishwa kwa
Msajili wa Mahakama Kuu, Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam Mhe. Salma Maghimbi
aliwataka Wasajili hao kuongeza kasi ya usimamizi wa kazi za Mahakama kwa kuwa
Mahakama tayari imepiga hatua kubwa kiteknolojia.
Alisema Usimamizi wa kazi za Mahakama hauna budi kuwa
mzuri ili mafanikio ya kiteknolojia yaendane na uwekezaji mkubwa uliofanywa na
Mahakama ya Tanzania.
Wasajili wapya walioapishwa ni Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya ambaye aliapishwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Chiganga
Mashauri Tengwe aliyeapishwa na Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni