Na. Richard Matasha-Mahakama, Mtwara
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim amewahimiza watumishi wa Mahakama katika Kanda hiyokufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati na viwango vilivyowekwa.
Mhe. Rose ametoa wito huo hivi karibuni alipokuwa kwenye ziara ya kukagua shughuli za kimahakama katika Mahakama ya Wilaya Newala.
Jaji Mfawidhi alielekeza kazi ziendelee kufanyika kama inavyotakiwa wakati changamoto zinazobainishwa zikishughulikiwa katika ngazi mbalimbali.
Aliwataka Mahakimu wote kuondoa na kuzuia mashauri ya mlundikano, mashauri kuendelea kuendeshwa kwa njia ya mtandao (eCMS) kwa Mahakama ya Wilaya na kuyahuisha kwenye mtandao kwa Mahakama za Mwanzo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Rose alipata fursa ya kupanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama ikiwa ni sehemu ya kutunza mazingira.
Awali, akisoma taarifa yake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Newala, Mhe. Innocent Sotter alimweleza Jaji Mfawidhi hali ya watumishi wa Mahakama, majengo na miradi iliyopo, mashauri, matumizi ya TEHAMA, bajeti na changamoto zinazoikabili Mahakama hiyo.
Katika ukaguzi huo, Jaji Mfawidhi aliongozana na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Seraphine Nsana, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mnzava na Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Bw. Richard Mbambe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni