Jumatano, 3 Aprili 2024

BODI YA UDHAMINI WA TAARIFA ZA JUZUU LA SHERIA TANZANIA YAKUTANA

Na Tawani Salum-Mahakama Dodoma

Bodi ya Jaji Mkuu wa Tanzania ya Udhamini wa Taarifa la Juzuu la Sheria Tanzania inaendelea na kikao chake cha siku tatu kuchambua maamuzi ya Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Tanzania Bara na Mahakama Kuu Zanzibar. 

Wakati wa kikao chake, Bodi inachambua maamuzi ya mwaka 2023 kwa Kitabu cha Toleo la Pili la Mwaka 2023 ([2023] Volume 2) na kuanza kuchambua maamuzi ya mwaka 2024 ili kuandaa Kitabu cha Mwaka 2024.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho kinachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya Midland jijini hapa, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Jacobs Mwambegele alisema kikao hicho ni cha mara ya kwanza  kufanyika mwaka 2024

Mhe. Mwambegele aligusia pia kuanza kutumika kwa Juzuu la Sheria la Mwaka 2007 hadi 2020 katika mfumo wa nakala laini (Online Law Reports 2007/2020) ili kuweza kuwafikia watumiaji wengi kwa kuwa machapisho ya nakala ngumu ni gharama na hayawafikii wengi. 

Bodi inakutana ikiwa tayari imekwishaandaa Taarifa ya Juzuu la Sheria Tanzania la Mwaka 2021 hadi Mwaka 2023, Toleo la Kwanza (TLRs 2021/2023 Volume 1) na katika kikao hiki tunakamilisha Taarifa ya Juzuu la Sheria Kitabu toleo l pili kwa Mwaka 2023 ([2023] Volume 2) na kuanza Kitabu cha Mwaka 2024,” alisema Mhe. Mwambegele.

Aliongeza kuwa Bodi hiyo katika kikao kijacho itaendelea na  Taarifa ya Juzuu la Sheria kwa Mwaka 2024, lengo ni kutoa kitabu cha Juzuu la Sheria kila baada ya robo mwaka kwa kipindi kijacho.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mratibu wa Bodi, Mhe. Kifungu Kariho alisema kuwa upatikanaji wa maamuzi katika Bodi umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani mengi yanapatikana kwenye Mfumo wa Mahakama unaochapisha Maamuzi, Sheria na Kanuni bure mtandaoni (TanzLII)

“Kwa kipindi kijacho cha miaka miwili, zoezi hili litarahisishwa zaidi baada ya muunganiko wa Mfumo wa Kielektroniki wa Mashauri wa Mahakama, Maktaba Mtandao pamoja na Mfumo wa TanzLII na kuongeza kasi ya kuchambua maamuzi hayo. Lengo la Bodi ni kutoa Kitabu cha Juzuu la Sheria mara nne kwa mwaka, yaani kila baada ya robo mwaka,” Mhe. Kariho alisema.

Bodi hiyo ina wajumbe 11, ambao ni Majaji kutoka Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu kwa upande wa Bara na Zanzibar, Mawakili kutoka Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoka Bara na Zanzibar na uwakilishi wa Vyama vya Mawakili Tanzania Bara na Zanzibar

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. DktJuliana Massabo (aliyesimama) akiwakaribisha wajumbe wa Bodi ya Jaji Mkuu wa Tanzania ya Udhamini wa Taarifa  za Juzuu la Sheria Tanzania katika ukumbi wa mkutano uliopo Midland Hoteli Jijini Dodoma.

Katibu wa Bodi hiyo, Prof. Hamudi Majamba akisisitiza jambo kwa wajumbe waliohudhuria kikao hicho.

Wajumbe wa bodi hiyo wakifuatilia kwa umakini kikao hicho.


Wajumbe wa bodi hiyo wakiwa katika picha ya pamoja wakiongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele.

(Picha na Arapha Rusheke-Dodoma)

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni