· Yawika mwaka 2023
· Kufanya makubwa tena 2024
· Jaji Mfawidhi aeleza siri ya mafanikio
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina jana tarehe 3 Aprili, 2024 ameongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama hiyo kujadili mambo mbalimbali ya kiutumishi na kufanya tathmini ya utendaji kwa mwaka 2023.
Kikao hicho kilichofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni kilihudhuriwa pia na Viongozi waandamizi wa Mahakama hiyo, akiwemo Naibu Msajili Mwandamizi, Mhe. Enock Matembele, Naibu Msajili Mary Mrio na Mtendaji, Bw, Jumanne Muna na wawakilishi kutoka Chama cha Wafanyakazi TUGHE Mkoa na Mahakama Makao Makuu.
Akizungumza wakati akifungua Kikao hicho, Mhe. Dkt. Mlyambina alieleza kuwa mwaka 2023 ulikuwa wenye mafanikio makubwa na siri kubwa ni kushirikisha watumishi ambao walionesha umahiri mkubwa katika ubunifu, hivyo kuimarisha utendaji wao wa kazi.
Alibainisha kuwa walipokea ushauri kutoka kwa mtumishi wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuhusu kuanzishwa wa sheria za kazi kiganjani, yaani Labour Laws Mobile App, ambazo zilizinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 29 Septemba, 2023.
“Sambamba na uzinduzi huo, tarehe hiyo hiyo tulizindua Juzuu za Sheria za Kazi za maamuzi ya Mahakama ya Rufani, toleo la kwanza. Kadhalika tulifanya uzinduzi wa mkusanyiko wa sheria za kazi pamoja na kanuni zake, yaani Principal and Subsidiary Legislations, ambazo zote zimewekwa kwa pamoja,” Jaji Mfawidhi alisema.
Alieleza kuwa kufuatia uzinduzi huo baada ya kufuata maelekezo ya Jaji Mkuu, nyaraka laini za Juzuu hizo ziligawanywa kwa kila mdau wa Mahakama ya Kazi bure, ikiwemo Shule ya Sheria kwa Vitendo, Vyuo Vikuu na wadaau wengine kama Mawakili.
Mhe. Dkt. Mlyambina alibainisha vile vile kuwa mtumishi kutoka Kitengo cha Uhasibu alishauri kuanzishwa kwa Kamati ya Elimu ambayo imekuwa ikitoa elimu kwa watumishi wa Mahakama nchini na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na imekuwa ikifanya hivyo kwa njia ya kielektroniki.
“Katika mwaka huu wa 2024, tunategemea pia kushirikisha zaidi watumishi na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma kwa Wadau na jamii kwa ujumla. Miongoni mwa vipaumbele tulivyonavyo katika matumizi ya TEHAMA ni kuanzisha Jukwaa la Jumuiya ya Sheria za Kazi Tanzania, yaani Tanzania Labour Law Community Forum,” alisema.
Jaji Mfawidhi alifafanua kuwa Jukwaa hilo litakuwa kwa ajili ya Wadau wa sheria za kazi ambalo litawapa nafasi Wawekezaji nchini kutoa maoni yao mbalimbali, kwani hadi sasa hawana jukwaa kama hilo, kwa maana ya sheria zinazohusu kazi.
“Tunategemea katika jukwaa hili mambo yote yanayohusiana na masuala ya sheria za kazi yatapata nafasi ya kujadiliwa na Wadau wote ndani na nje ya Nchi. Hata Mwekezaji akiwa Marekani, ikiibuliwa hoja ya kujadili mambo ya sheria za kazi atapata fursa na yeye ya kufanya hivyo,” alisema.
Mhe. Dkt. Mlyambina alieleza pia kuwa kutakuwa na watu katika Jukwaa hilo ambao watakuwa wanaibua hoja ili kila mtu aweze kuchangia na wameona ushirikishaji wa watumishi unawapa nafasi ya kuwa wabunifu zaidi na kuleta mambo yenye tija, siyo tu kwa Divisheni ya Mahakama Kuu Kazi na Mahakama ya Tanzania kwa ujumla, bali pia kwa Taifa.
Kadhalika, Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa kwa mwaka wa 2024 wanatazamia kutengeneza Kanuni za Uwakilishi Binafsi, yaani Personal Representative Rules, kwani tangu Mahakama Kuu Kazi imeanza mwaka 2007, miaka takribani 17 hadi sasa, wapo Wawakilishi Binafsi, lakini hawathibitiwi kwa kutokuwepo kanuni zozote zinazowaongoza katika utendaji wao wa kazi.
“Matokeo yake kumeibuka malalamiko kwa baadhi yao, wengine kutofanya vizuri au kutokufanya kazi zao bila kufuata maadili. Tumeona ni muda muafaka kwa sasa, lazima tuwe na kanuni zitakazowaongoza Wawakilishi Binafsi ambao wanatambulika kisheria,” alisema.
Mhe. Dkt. Mlyambina alieleza kuwa kanuni hizo zitawaongoza kufanya kazi zao kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na utaratibu huo utawabana wale ambao wanajipachika kuwa Wawakilishi Binafsi wakati hawana sifa.
Alisema kwamba kutokana na uzoefu wameshuhudia Wanafunzi ambao hawafauru katika Shule ya Sheria kwa Vitendo au kwenye vitivo mbalimbali vya sheria na pia Mawakili ambao hawahuishi leseni zao hukimbilia kuwa Wawakilishi Binafsi.
“Mwaka huu 2024 lazima tuzitengeneze hizi kanuni na bahati nzuri Jaji Mkuu wa Tanzania ametupa maelekezo kuhakikisha jambo hili linafanyika na kupewa kipaumbele…
“Mpaka sasa, tumeshaunda kamati inayohusiana na Wawakili Binafsi. Tumeunda pia kamati inayohusiana na Jukwaa na tayari wameanza kufanyia kazi. Wameshaleta rasimu kwenye hii ya Wawakilishi Binafsi, tunatazamia kuiboresha na kuipeleka mbele ya Kamati ya Jaji Mkuu na kuwashirikisha Wadau mbalimbali,” Jaji Mfawidhi amesema.
Mhe. Dkt. Mlyambina aliendelea kubainisha kuwa mwaka huu wa 2024 pia wanatazamia kuwa na Juzuu za maamuzi ya Mahakama Kuu Kazi, toleo la kwanza kwa nchi nzima. Alisema kuwa hatua hiyo itawapa Wananchi wigo mpana wa kusoma na kuelewa vizuri sheria za kazi, misimamo na maamuzi ya Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani.
Kadhalika, alisema Kamati ya Elimu itaendelea kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria ili wananchi wawe na uelewa mpana juu ya sheria za kazi na hivyo kupunguza malalamiko kuja mahakamani, lengo ni kuzuia kuletewa migogoro mingi kwa watu kutokuwa na uelewa.
“Tusipowapa watu uelewa wa sheria za kazi, taratibu na kanuni za kuleta migogoro yao itakuja migogoro mingi ambayo haina msingi au migogoro mingine inakuja bila kufuata taratibu. Ukiwapa elimu hii kikamilifu utapunguza utitiri wa migogoro, hivyo kutopoteza muda mwingi mahakamani,” Jaji Mfawidhi alisema.
Wakati wa Kikao hicho, wajumbe wa Baraza walipokea pia taarifa ya utendaji iliyowasilishwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kazi, ambaye alieleza kuwa Divisheni hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kutumia ubunifu katika kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza.
Bw. Muna alieleza pia kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Mahakama hiyo ilipokea fedha za amana jumla ya Shilingi za Kitanzania 2,261,463,895.79 kutoka kwa Wadau kwenye mashauri mbalimbali yaliyosikilizwa.
Alibainisha kuwa jumla ya fedha kiasi cha Shilingi za Kitanzania 1,931,651,252.55 zimelipwa kwa washinda deni tuzo baada ya mashauri yao kumalizika, huku kiasi kilichobaki cha Shilingi za Kitanzania 329,812,143.24 kikiwa kwenye akaunti ya amana na fedha hizo zitashughulikiwa baada ya wahusika kikamilisha taratibu za malipo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni