Alhamisi, 2 Mei 2024

WATUMISHI MAHAKAMA KUU BUKOBA WAMUAGA MSAIDIZI WA OFISI MKUU

Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba

Watumishi wa Mahakama Kuu Bukoba mkoani Kagera hivi karibuni walifanya hafla fupi ya kumuaga Msaidizi wa Ofisi MkuuBw. George Ntakulega baada ya kustaafu kwa umri mwezi Aprili, 2024.

Hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Bukoba iliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya TanzaniaKanda ya Bukoba, Mhe Immaculta Banzi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Banzi alimshukuru Bw. Ntakulega kwa kipindi chote walichofanya kazi na kubainisha kuwa kuna mengi wamejifunza kutoka kwake na kumtakia kila lililo kheri kwenye majukumu yake mapya katika ustaafu.

Naye Bw. Ntakulega aliwaasa watumishi wenzake kuendelea kudumisha upendo, uwajibikaji na ushirikiano baina yao ili kutimiza majukumu yao na kuleta matokeo chanya katika kazi zao za kila siku. 

“Napenda kuwashukuru Viongozi wangu na watumishi wenzangu kwa muda wote tuliokuwa pamoja hapa kazini. Naomba kuwaachia maneno mafupi nayo ni kudumisha upendo, uwajibikaji na ushirikiano,” alisema.

Viongozi wengine waliokuwapo katika hafla hiyo ni Majaji wa Mahakama Kuu Bukoba, Mhe. Emmanuel Ngigwana, Mhe. Ayub Mwenda na Mhe. Gabriel Malata, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe. Odira Amworo na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko.

Kwa upande wake, Bw. Simkoko alisisitiza watumishi kufanya kazi kwa bidii wote na kumtakia Bw. Ntakulega kila la kheri katika shughuli nyingine katika kustaafu kwake, ikiwemo ufugaji na ukulima.

Bw. George Ntakulega akipokea zawadi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi na Majaji Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba.

Mtaafu Bw. George Ntakulega akionyesha zawadi alizopokea kutoka kwa Majaji wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Bukoba.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko akitoa neno fupi kwa mtaafu pamoja na watumishi wengine.

 

 Mtaafu Bw. George Ntakulega akipokea zawadi kutoka kwa Bi Amina Juma Msaidizi wa Hesabu Mahakama Kuu Bukoba.

 Mtaafu Bw. George Ntakulega akifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa hafla hiyo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni