Alhamisi, 2 Mei 2024

HAKI INAENDANA NA WAJIBU; MPANGO

·      Serikali yaahidi mema kwa Wafanyakazi siku za karibuni

 

Na Seth Kazimoto - Mahakama Kuu Kanda ya Arusha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amewataka Wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwakuwa haki inaendana na wajibu

 

Akizungumza na wafanyakazi lukuki waliofurika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani jana tarehe 01 Mei, 2024, Mhe. Dkt. Mpango aliwataka wafanyakazi wasiochapa kazi ipasavyo wajitafakari vizuri kama kweli wanastahili kubakia katika nafasi walizonazo.

 

“Haki inaendana na kutimiza wajibu, hivyo wafanyakazi wote hamna budi kuchapa kazi kwa bidii wakati Serikali inaangalia uwezekano wa kuboresha maslahi yenu,” alisema Makamu wa Rais.

 

Awali, akisoma hotuba ya wafanyakazi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Bw. Henry Mkunda alibainisha maeneo kadhaa ambayo yanamkandamiza Mfanyakazi kwa namna moja au nyingine.

 

Aliyataja maeneo hayo ambayo ni pamoja na  maboresho ya mishahara ya nyongeza ya mshahara ya asilimia 23 yaliyofanywa mwaka 2023 hayakugusa wafanyakazi wote wa Serikali kwa asilimia hizo, wafanyakazi wengine walipata nyongeza ya asilimia kidogo.

Bw. Mkunda ameiomba Serikali kuongeza asilimia 23 ya mshahara kwa wafanyakazi wote na si baadhi yao, huku akieleza kuwa, hali hiyo imerudisha nyuma morali ya kufanya kazi kwa wafanyakazi kwani nyongeza hiyo ilikuwa ya kibaguzi kwa baadhi ya Wafanyakazi.

 

Kadhalika, Bw. Mkunda alitaja maeneo mengine yenye ukakasi kwa wafanyakazi kuwa ni suala la Kikokotoo, kubadilishwa kwa vitita vya bima ya afya, huduma duni za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), likizo ya uzazi kwa wafanyakzi wa kike wanaojifungua watoto njiti na tatizo la kutolipwa mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi katika Halmashauri mbalimbali kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Halmashauri husika.

 

Akizungumzia suala la kikokotoo, Bw. Mkunda alisema kuwa Kanuni inaotumika kulipa mafao kwa wafanyakzi wanaostaafu si nzuri kwa sababu inanyima Mtumishi kulipwa mafao yenye staha na matokeo yake wastaafu na kulipwa malipo kidogo na kuanza kuishi maisha duni, hali ambayo inawaondolea hadhi na heshima katika jamii. 

 

TUCTA imeiomba serikali kufanya maboresho ya Kanuni ya kukokotoa mafao ya mstaafu ili wafanyakazi wanufaike na jasho lao.

 

Vilevile, Bw. Mkunda amelalamikia kitendo cha Serikali kubadili vitita vya Bima ya Afya bila kushirikisha wanachama wa mfuko huo ambao ni wafanyakazi. Ameongeza kwamba, mabadiliko hayo yamepunguza kiwango cha huduma zilizokuwa zinapatikana kabla ya mabadiliko, hali ambayo inawaathiri moja kwa moja wafanyakazi ambao ndio watumiaji wa vitita hivyo. 

Kuhusiana na huduma ambazo si nzuri za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), TUCTA imesema kuwa, idadi ya watumishi ni ndogo na vitendea kazi ni vichache na havikidhi mahitaji hali ambayo inachelewesha migogoro ya kikazi inayopelekwa hapo ili itatuliwe, na hivyo kusababisha ucheleweshwaji wa haki za wafanyakazi ambao wamepeleka mashauri yao ili yapatiwe ufumbuzi kwa wakati.

 

Bw. Mkunda, ameiomba Serikali kuongeza likizo ya uzazi kwa wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti ili kuwawezesha akina mama hao kuweza kupona vizuri na pia kuwapa uangalizi watoto wao ipasavyo.

 

Akijibu hoja zilizoibuliwa na TUCTA, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametolea ufafanuzi hoja mbalimbali ikiwemo suala la nyongeza ya mshahara ya asilimia 23, ambapo alisema, asilimia hizo zililenga wafanyakazi wenye mishahara midogo na wafanyakazi wengine waliguswa na nyongeza hiyo kwa asilimia chini ya 23 kulingana na ukubwa wa mshahara.

 

Mhe. Dkt. Mpango aliongeza kuwa, Serikali imesikia na kupokea ushauri uliotolewa kuhusiana na kikokotoo kilivyo kwa sasa na kwamba Serikali inawahakikishia kuwa, haipendi kuona wastaafu wanataabika, hivyo serikali inaendelea kufanya tathmini ya kina toka kwa watakwimu bima ili kupata ufumbuzi.

 

Kwa upande wa likizo ya uzazi kwa wafanyakazi wa kike wanaojifungua watoto njiti, Makamu wa Rais alisema kuwa kuanzia sasa, kipindi cha uangalizi maalum wa mtoto hakitahesabiwa kama likizo ya uzazi, na likizo itaanza pale ambapo hali ya mtoto itaimarika. Mfanyakazi huyo atakuwa anatoka kazini saa saba na nusu mchana kwa kipindi cha miezi sita.

 

Kuhusu watumishi walioajiriwa na Halmashauri ambao uhakika wa kulipwa mshahara ni mdogo, Serikali imeshalipokea na kuanza kulifanyia kazi ambapo alisema hadi kufikia sasa, jumla ya watumishi 473 tayari wameingizwa katika taratibu wa kulipwa na Serikali Kuu.

 

Aidha, Makamu wa Rais amewahimiza wafanyakazi wote kuendelea kujenga utamaduni wa kudai risiti kila wanaponunua bidhaa mbalimbali ili kuisaidia Serikali kukuza mapato. Ameongeza kwa kusema kuwa, kama hali ya uchumi itaendelea kuwa nzuri, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atatoa tamko la nyongeza ya mshahara hivi karibuni. 

 

Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ni miongoni mwa Wafanyakazi walioshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Arusha. 

 

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Tulia Ackson, Naibu Waziri Mkuu na Mawaziri kadhaa. Pia walikuwepo Viongozi kadhaa wa Mahakama wakiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (katikati) akiwa katika meza kuu. Wa pili kushoto ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Akson (kulia), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi (kushoto) na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Tumaini Nyamhokya wakiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa Jijini Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana tarehe 01 Mei, 2024.

Wafanyakazi wa Mahakama wakishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana tarehe 01 Mei, 2024.



Sehemu ya umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa Jijini Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana tarehe 01 Mei, 2024.


(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni