Alhamisi, 2 Mei 2024

MEI MOSI YAFANA KIGOMA

Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma

 

Mkuu wa Mkoa Kigoma,  Mhe. Thobias Andengenye, ameongoza wafanyakazi wa idara tofauti za binafsi na Serikali kusherehekea siku ya wafanayakazi duniani tarehe 1, May 2024.

 

Akizungumza katika sherehe hizo, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya maboresho makubwa ya stahiki za wafanyakazi ikiwa ni kuondoa kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili kupitia sera na sheria mbalimbali.

 

Amesema kuwa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi yatumike kushughulikia changamoto za wafanyakazi na kumkomboa kikamilifu mfanyakazi katika nyanja zote za kazi ili apate stahiki zake zote bila kupunjwa kwa namna yoyote.

 

Hata hivyo,  Mhe. Andengenye alisema kuwa yapo mambo ambayo waajiri kwa nafasi yao wanapaswa kushughulikia kwa haraka na ametoa wito kwa waajiri kutimiza wajibu wao kwa kushughulikia stahiki za wafanyakazia na kuondoa changamoto zinazojitokeza mahala pakazi.

 

Serikali inaendelea kuongeza mapato yake yanayotokana kodi mbalimbali, sote tunafahamu kuwa Serikali inapokuwa na mapato ya kutosha ndivyo inavyopata uwezo wakuwalipa vizuri wafanyakazi wake, amesema.

 

Kwa upande wake, Katibu wa Shirikisho la Vyama  vya Wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Kigoma, Bw. Jumanne Magulu, akisoma risala kwa niaba ya vyama vya wafanyakazi Kigoma alisema, “Wafanyakazi mkoani Kigoma wanaipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanyia kazi changamoto za wafanyakazi, hali iliyosababisha kulipwa kwa stahiki nyingi za wafanyakazi.

 

Magulu alimpongeza Rais Samia kwa upandishaji wa madaraja kwa watumishi wa umma, kupunguza muda wa upandishaji madaraja na kuondolewa kwa tozo ya asilimia sita ya mikopo kwa waliokuwa wanafunzi wa elimu ya juu.

 

Hata hivyo, alianisha baadhi ya changamoto katika upatikanaji wa stahiki zao za madai mbalimbali,ikiwemo nyongeza za malipo ya wastaafu wa muda mrefu ambao wamekuwa wakilipwa mafao kidogo ambayo hayaendani na hali halisi ya maisha ya sasa. Aliomba kurekebishwa kwa kikokotoo cha mafao kilichopo sasa ili kirudishwe kile cha awali.

 


 Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye akizungumza katika sherehe ya Mei Mosizilizofanyika katika uwanja wa Umoja ulipo Mjini Kasulu Kigoma.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe Rose Kangwa akitoa cheti kwa wafanyakazi hodari wasio wanachama wa Tughe katika hafla fupi baada ya sherehe za Mei Mosi. Anaepokea cheti ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Uvinza, Mhe. Frank Mtega aliyeibuka Mfanyakazi Bora kutoka Mahakama ya Wilaya Uvinza.

 

Baadhi ya Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Kigoma. Aliyesisimama ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kasulu Mjini, Mhe. Rajabu Mtuli (kulia), akifatiwa na Afsa Tawala wa Wilaya ya Kibondo, Bi. Naomi Chawe. Kushoto) wa kwanza ni Msaiduizi KumbukumbuBi. Witness Mutayoba, akifuatiwa na Mwandishi Mwendesha Ofisi, Bi. Rachel Kamaze na aliyechuchumaa ni Afisa Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Bw. Hansi Joramu.


Wafanyakazi wa Mahakama Kigoma wakiwa katika sherehe za Mei Mosi wakifuatilia hotuba ya Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,  Mhe. Thobias Andengenye. Kulia) ni Hakimu Mkazi Mahakama Wilaya ya Kigoma, Mhe Anna Kahungu, aliyevaa miwani na kofia ya Tughe (kushoto) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ujiji, Mhe. Vestina Nombo.


Picha ya wafanayakazi wa Mahakama wakiimba wimbo wa mshikamano katika sherehe za Mei Mosi zilizofanyika katika uwanja wa Umoja ulipo Kasulu Mjini, aliyevaa kofia nyeupe ni Hakumu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Ujiji-Kigoma Mhe. Hassan Galiatano.


Picha ya wafanayakazi wa Mahakama Kigoma wakiwa katika maandamano ya sherehe za Mei Mosi wakiwa na bango maalumu lenye ujumbe wa siku ya sherehe ya wafanyakazi duniani.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Maoni 1 :