Na Mwanaidi Msekwa-Mahakama Kuu, Kazi
Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi jana tarehe 7 Mei, 2024 iliendesha mafunzo kwa Viongozi na watumishi wote kuwajengea uelewa kuhusu Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma (PEPMIS & PIPMIS).
Viongozi waliohudhuria mafunzo hayo ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga na Naibu Wasajili, Mhe. Enock Kassian, Mhe. Mary Mrio na Mhe. Ritha Tarimo.
Mtoa mada katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo kwenye jengo la Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Kinondoni Dar es Salaam alikuwa Bw. Abdallah Omar Abdallah (Mchumi) kutoka Ofisi ya Rais-Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
Bw. Abdallah aliwapitisha watumishi katika matumizi sahihi ya Mfumo wa PEPMIS kwa kuanza na hatua za usajili hadi jinsi ya kuingiza taarifa za mpango kazi wa Taasisi na taratibu zote za kukamilika kwa kufuata muda uliopangwa kwa makubaliano ya wazi kati ya mwajiri na mwajiriwa kwa lengo la kuongeza ufanisi na uwazi zaidi.
Akizungumza baada ya kutolewa mafunzo hayo, Mhe. Dkt. Mlyambina alimshukuru Bw. Abdallah kwa kukubali mwaliko wa muda mfupi na kuja kutoa mada kwa weledi wa hali ya juu. Alimuomba kurudi tena kwa ajili ya mafunzo ya vitendo ili watumishi waweze kujifunza zaidi.
Awali, akizungumza wakati wa ufunguzi, Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Bi. Beatrice Dominic aliwaasa watumishi kusikiliza na kujifunza kwa makini kwa kuwa mfumo huo utatumika kupima utendaji wa kazi kila siku tofauti na utaratibu waliokuwa wanatumia hapo awali.
Hivi karibuni Serikali ilifanya mageuzi ya kiutendaji kwa kusanifu na kujenga Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma.
Hii ni kutokana na Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008, Sheria ya Utumishi wa Umma Sura Na. 298, Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 na miongozo mingine.
Kwa nyakati tofauti, Serikali imekuwa na utaratibu wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi za Umma ili kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma, utoaji wa huduma bora, ufanisi na tija katika kutekeleza malengo ya kila Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Mfumo wa PEPMIS & PIPMIS umeandaliwa kwa kuzingatia dhana ya uwajibikaji wa hiari katika kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kwa kuzingatia uhitaji mkubwa wa wananchi wa kupata huduma bora na kwa haraka.
Mfumo pia umeandaliwa kwa kuzingatia kasi kubwa ya ukuaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika nyanja zote za uzalishaji mali na utoaji wa huduma. Uazishaji wa Mfumo huu utapelekea kuleta utendaji kazi wenye tija na unaojali matokeo katika Taasisi za Umma.
Kutoka katika Mwongozo huo, Katibu Mkuu Utumishi amewataka waajiri kusimamia watumishi katika kuandaa mipango ya utendaji kazi; kufuatilia utekelezaji wa mipango ya utendaji kazi; kufanya mapitio ya mipango ya utendaji kazi; kutathmini utekelezaji wa mipango ya utendaji kazi ya mwaka na kutoa mrejesho wa utendaji kazi katika kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji.
Bw. Abdallah Omar Abdallah akitoa mada ya matumizi sahihi ya mfumo wa PEPMIS.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina. Viongozi wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga, Naibu Msajili Mfawidhi, Mhe. Enock Kassian, Naibu Msajili, Mhe. Mary Mrio, mtoa mada, Bw. Abdallah Omar Abdallah na Watumishi wa Divisheni ya Kazi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni