Alhamisi, 13 Juni 2024

NATARAJIA MUANZE KAZI KWA KASI – JAJI KIONGOZI

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Majaji watatu wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania walioapishwa leo wametakiwa kuanza kazi kwa kasi sambamba na kuunga mkono matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yaliyotamalaki ndani ya Mahakama ili kutoa haki kwa wananchi kwa wakati.

Akizungumza na Majaji hao pamoja na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 13 Juni, 2024 ofisini kwake jijini Dodoma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amesema anatarajia Majaji hao waanze kazi kwa kasi ya kukimbia.

“Natarajia muanze kazi kwa kukimbia, muwe kama Askari wanaoshuka chini na parachuti ambao mwendo wao hata baada ya kushuka chini ni wa kasi, hivyo muwe wepesi kujifunza kwa haraka ili tuweze kusonga mbele,” amesema Mhe. Siyani.

Jaji Kiongozi amesema kuwa, Majaji hao wameanza kazi wakati mzuri ambao ni katikati ya mwaka, hivyo ni rahisi kuwapima katika kipindi hiki cha miezi sita iliyobaki kuhitimisha mwaka.

Aidha, Mhe. Siyani amesema kwamba, ongezeko la Majaji hao anaamini kuwa litaenda sambamba na uharaka wa upatikanaji wa haki kwa kuwa mzigo wa mashauri kwa Majaji wa Mahakama unaendelea kushuka.

“Hadi kufikia mwisho wa mwaka 2023 wastani wa mzigo wa mashauri kwa kila Jaji ilikuwa ni 307, hivyo ongezeko la Majaji wapya wanne pamoja na mwingine aliyeapishwa mwezi Aprili litapunguza mzigo wa mashauri kwa kila Jaji na kufanya kuwa 298,” ameeleza Jaji Kiongozi.

Kadhalika, Mhe. Siyani amewaasa Majaji hao kuzifahamu na kuziishi Kanuni za Maadili za Maafisa Mahakama. “Mmeshakuwa Majaji, kuanzia sasa mjue  nyenendo zenu zinafuatiliwa, mnapaswa kuyaishi maisha yanayoakisi maadili, tupo kwenye zama ambazo kosa moja tu linaweza kuharibu taswira ya Mahakama nzima,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa, Kiongozi sio tu hapaswi kukiuka maadili lakini pia hapaswi kutiliwa mashaka ya kutokuwa na maadili hivyo ni muhimu kuzingatia hayo pamoja na kuziishi tamaduni mbalimbali za Mahakama.

Vilevile, Jaji Kiongozi amewataka Majaji hao kufanya kazi vizuri na watumishi walio chini yao, ambapo amesema, “mnalo jukumu la kulea Wasaidizi waliopo chini yenu, mnapaswa kuwaandaa kuwa watu ambao watapokea vijiti vyenu kwa kuwa Nchi ya kesho yetu inategemea sana kizazi tunachokiandaa sasa.”

Katika mazungumzo hayo, Majaji kadhaa wa Mahakama Kuu walioshiriki wamepata fursa ya kuzungumza na Majaji wapya na kuwapa uzoefu na ushauri wa utekelezaji wa majukumu ya Ujaji. Wote kwa ujumla wamewakaribisha na kuwasisitiza Majaji hao kutoa haki, ushirikiano pamoja na kuwa tayari kujifunza.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Laurent Masabo amewasihi Majaji hao kufanya kazi kwa kumpendeza Mungu kwa kuwa nafasi hiyo ni ya kipekee.

“Kazi ya kuhukumu ni kazi ya Mwenyezi Mungu, tunapaswa kufanya kazi hii kama Mwenyezi Mungu anavyotutaka,” amesema Mhe. Dkt. Masabo na kuongeza kwa kuwaomba Majaji hao kushirikiana na Majaji wenzao pamoja Naibu Wasajili, Makarani na watumishi wengine ili utendaji wao uwe rahisi.

Mhe. Dkt. Masabo amewasihi pia Majaji hao kuwa tayari kujifunza ambapo ameeleza kuwa hawapaswi kuona aibu kuuliza au kupata ushauri kutoka kwa Majaji wenzao juu ya namna bora ya kufanya vizuri zaidi katika kazi.

Majaji hao, Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania pamoja na Viongozi wengine wa Serikali walioteuliwa kushika nafasi mbalimbali wameapishwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Majaji walioapishwa leo ni Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza, Mhe. Mariam Mchomba Omary na Mhe. Nehemia Ernest Mandia. Aidha, Mhe. George Hillary Herbert naye ameapishwa kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Laurent Masabo (wa kwanza kulia) na Majaji watatu wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania walioapishwa leo tarehe 13 Juni, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akizungumza na Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Msajili wa Mahakama ya Rufani (hawapo katika picha) ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Laurent Masabo akizungumza na Majaji wapya wa Mahakama Kuu (hawapo katika picha) walioapishwa leo tarehe 13 Juni, 2024 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha akizungumza (aliyesimama kulia) jambo katika kikao kati ya Jaji Kiongozi na Majaji wapya pamoja na Msajili wa Mahakama ya Rufani walioapishwa leo tarehe 13 Juni, 2024 jijini Dodoma.
Sehemu ya Wasajili na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika mazungumzo kati ya Jaji Kiongozi na Majaji wapya na Msajili wa Mahakama ya Rufani walioapishwa leo tarehe 13 Juni, 2024.
Mazungumzo yakiendelea.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akimuapisha Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 13 Juni, 2024 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akimuapisha Mhe. Mariam Mchomba Omary kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 13 Juni, 2024 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akimuapisha Mhe. Nehemia Ernest Mandia kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 13 Juni, 2024 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akimuapisha Mhe. George Hillary Herbert kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 13 Juni, 2024 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani  (kushoto) akimkabidhi zawadi ya ua Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza ambaye ameapishwa leo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani  (kushoto) akimkabidhi zawadi ya ua Mhe. Mariam Mchomba Omary ambaye ameapishwa leo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
 
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani  (kushoto) akimkabidhi zawadi ya ua Mhe. Nehemia Ernest Mandia ambaye ameapishwa leo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
 
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani  (kushoto) akimkabidhi zawadi ya ua Mhe. George Hillary Herbert ambaye ameapishwa leo kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni