Jumatano, 12 Juni 2024

WAJUMBE KAMATI ZA MAADILI YA MAAFISA MAHAKAMA GEITA WAAPISHWA

 ·       Yumo Mkuu wa Mkoa Geita na Mkuu wa Wilaya hiyo

  Na Charles Ngusa , Mahakama, Geita.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Venance Mwakapeje amewaapisha wajumbe wa kamati mbili za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mkoa wa Geita, moja ikiwa ni ya Mkoa na nyingine ni ya Wilaya ya Geita.

 Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa walioapishwa ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Bw. Martin Sahigela (Mwenyekiti), Katibu Tawala wa Mkoa huo (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Mkoa, Maafisa wawili wa Mahakama wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.

 Kwa upande wa Kamati ya Maadili ngazi ya wilaya walioapishwa ni Mkuu wa wilaya ya Geita, Bw. Hashim Komba (Mwenyekiti), Katibu Tawala wa wilaya hiyo (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa wilaya pamoja na Mahakimu wawili walioteuliwa na Jaji Mfawidhi.

 Akizungumza Tarehe 10 Juni, 2024 mara baada ya kuapishwa, Mkuu wa Mkoa wa Geita na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa alisema kuwa ni wakati muafaka kwa Kamati yake kufanya kazi ili kutekeleza majukumu yao ya msingi kama ilivyokusudiwa kuanzishwa kwa kamati hizo.

 ”Ni wakati sasa Wajumbe wa kamati hii kuwa na mtazamo wa mbali zaidi na wasiishie kujadili Maadili ya Mahakimu tu bali pia waje na mawazo mapya ya kuangalia pia mazingira na miundombinu wanayofanyia kazi na kuja na mkakati wa kuiboresha ili iwe rafiki na isiwe kichocheo cha ukiukwaji wa Maadili”, alisema  Mkuu wa Mkoa.

 Aidha, amewataka wajumbe wa Kamati ya Mkoa kujiepusha na migogoro kati ya Mihimili ya Dola inayoweza kutokea wakati Kamati ikitekeleza majukumu yake ili kutoathiri shughuli za utoaji haki.

 ”Baada ya kuapishwa, sasa Kamati hizi zitaweza kufanya kazi kwa weledi na kwa mujibu wa sheria na pia  zitakuwa na mtazamo wa kujenga zaidi”, alisisitza Mkuu wa Mkoa.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Geita ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Hashim Komba alisema kuapishwa kwa wajumbe wa kamati ya wilaya ni kuipa Kamati hiyo mamlaka kamili ya kufanya shughuli zake tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

 Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Wajumbe hao, Jaji Griffin amemuomba Mkuu Geita kusaidia kutoa elimu kwa wananchi  juu ya mauala mbalimbali ya kisheria ikiwemo sheria za mikopo ili kuepuka migogoro inayotokana na mikopo umiza.

Aidha, alimuomba Mkuu wa wilaya ya Geita asaidie kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali ili waweze kumalizia jengo la Mahakama Nyarugusu ili kuboresha utoaji huduma katika eneo hilo.

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 


Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Mkoa wa Geita na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Martin Shigela akizungumza mara baada ya kuapishwa Tarehe 10 Juni, 2024 mkoani humo.

(Habari hii imehaririwa na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama)

 

 

 

 

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni