Jumatatu, 3 Juni 2024

WALIMU SHULE YA SEKONDARI MWANALUGALI PWANI WAOMBA KUPATIWA ELIMU YA SHERIA

Na Eunice Lugiana, Mahakama Pwani

Walimu wa Shule ya Sekondari Mwanalugali iliyopo Kibaha Mkoa wa Pwani wameuomba Uongozi wa Mahakama Mkoa wa Pwani  kuipatiwa elimu ya Sheria ili nao waweze kuwaelimisha wanafunzi walioko katika Klabu ya Mahakama katika Shule hiyo. 

Akizungumza mwisho wa mwezi uliopita, wakati Viongozi wa Mahakama Pwani walipotembelea Shule hiyo, wakati wa kuuliza maswali katika Klabu hiyo, Mwalimu wa Shule hiyo, Bi. Prisca Kiondo alisema kila Alhamis shuleni hapo kumekuwa na Klabu za masomo mbalimbali kutokana na Mahakama kutoa elimu mara moja kwa mwezi.

Akijibu hoja hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Fahamu Kibona ambaye ni Mratibu wa Klabu ya Mahakama katika Shule hiyo, alisema licha ya kuwa, wanapaswa kufika mara moja kwa mwezi, amesema watapanga ratiba vizuri ili waweze kuhudhuria kila Alhamis na kutoa elimu katika Klabu hiyo. Na pia ameongeza kwamba, watapanga ratiba ya kuwaelimisha Walimu baadhi ya Sheria muhimu ili waweze kupata uelewa zaidi kuhusu ya Sheria.

Katika Klabu hiyo, Wanafunzi waliuza na maswali kadhaa ili kupata uelewa wa masuala ya Mahakama. Akiuliza swali mojawapo mwanafunzi wa kidato cha pili aliyejitambulisha kwa jina la Yumeni Aluta, aliuliza hatua gani zinazochukuliwa endapo Hakimu akipokea rushwa na kupindisha Sheria.

Akijibu swali hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi alisema, “sisi Mahakimu na Majaji ambao tunashughulika moja wa moja kutoa maamuzi katika suala la kwanza na la msingi kabisa ni sisi kuhakikisha kwamba tuko katika uadilifu kwa hiyo hatutakiwi kupokea au kushawishi rushwa.”

Alisema, kama ikitokea hivyo, ipo Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa, hivyo taarifa ya Mhusika aliyepokea rushwa inapaswa kutolewa huko na kama akikamatwa atashtakiwa kama watu wengine.

Aidha, Mhe. Mkhoi aliongeza kuwa, zipo Tume za Maadili kwa Mahakimu ambazo zinashughulikia masuala ya Maadili kwa Mahakimu, Tume hizo zipo katika ngazi za Wilaya, ngazi za Mikoa na mpaka ngazi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani. 

“Hivyo kama kuna viashiria vyovyote vya uvunjifu wa maadili kwa Maafisa hawa wa Mahakama Kamati hizo zitahusika kuchukua hatua stahiki,” alieleza Mfawidhi huyo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama Ya Hakimu Mkazi  Pwani , Mhe Joyce Mkhoi (kushoto ) pamoja na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe Emael Lukumai wakisikiliza maswali yaliyokuwa yakiulizwa na Wanafunzi wa Klabu ya Mahakama katika Shule ya Sekondari Mwanalugali (hawapo katika picha).

Wanafunzi wa Klabu ya Mahakama katika Shule ya Sekondari Mwanalugali iliyopo Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wakifuatilia Elimu iliyokuwa ikitolewa na Mahakimu (hawapo katika picha) wakati Mahakimu hao walipotembelea Shuleni hapo kutoa elimu ya Mahakama na Sheria kwa ujumla.

 
Hakimu Mkazi Wa Mahakama ya Wilaya Kibaha na Mratibu wa Klabu ya Mahakama katika Shule ya Sekondari Mwanalugali, Mhe. Fahamu Kibona (aliyesimama) akitoa ufafanuzi kufuatia ombi lililoombwa na Walimu wa Shule hiyo.


Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mwanalugali, Mwl. Prisca Kiondo akitoa Ombi la kupatiwa elimu kwa Walimu ili nao waweze kuwaelimisha wanafunzi.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)













Hakuna maoni:

Chapisha Maoni