Jumatatu, 3 Juni 2024

MAHAKAMA MBEYA YASHUHUDIA USIKU MWANANA IKIWAAGA VIONGOZI

Na Iman Mzumbwe-Mahakama, Mbeya

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda Mbeya ilifanya hafla ya kuwaaga viongozi wanne waliohama na kuwakaribisha viongozi wengine watano waliohamia Mahakama Kuu, Kanda hiyo wakiwemo Majaji watatu, Naibu Msajili mmoja (1) na Mtendaji wa Mahakama Kuu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru akiongoza hafla hiyo mwanana aliwakaribisha wageni waalikwa, wadau wa Mahakama, watumishi waliohama pamoja na wale waliohamia Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Vilevile Mhe. Ndunguru aliwashukuru Viongozi wote kwa kujitoa kwao wakati wote walipokuwa wanatekeleza majukumu yao na kuwapongeza viongozi hao kwa kutenga muda wao adhimu kuitikia wito wa kufika katika hafla hiyo ili kuwaaga rasmi.

“Haikuwa rahisi sana kuacha majukumu yenu ya msingi ya kuwahudumia wananchi na kutenga japo muda kidogo mkafika hapa kwa ajili ya jambo dogo kama hili hakika mmetuheshimisha kwa kuwa nasi hapa leo hii, tumefurahi kukutana nanyi wanafamilia wenzetu,” alisema Jaji Ndunguru.

Mhe, Dunstan Ndunguru aliwaeleza viongozi hao kwamba licha ya kuwaaga bado Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ni nyumbani kwao, hivyo aliwasisitiza kwamba wanapopata nafasi wasisite kufika ili wasalimie na kubadilishana mawazo na watumishi waliopo.

Hafla hiyo iliwajumuisha Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Waheshimiwa Naibu Wasajili, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mahakimu Mahakama zote za Mkoa wa Mbeya na Mkoa Songwe, watumishi wa Mahakama Mbeya na Songwe, pia wadau wa Mahakama wa Kanda nzima ya Mbeya. Mchaparo ho ulifanyika tarehe 31 Mei, 2024 katika ukumbi wa Beaco Resort Kadege Mbeya.

Viongozi walioagwa ni pamoja na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliyehamishiwa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es slaam Mhe, David Ngunyale, Naibu Msajili Mwandamizi Mhe, Projestus Kahyoza aliyehamia Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma na Mtendaji wa Mahakama Kuu Bw.Teoford Ndomba aliyehamia Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.

Wakati viongozi waliokaribishwa ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Mussa Kassim Pomo, Mhe. Emmanuel Kawishe, Mhe. Aisha Sinde, Naibu Msajili Mhe. Judith Lyimo pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti.

Aidha, viongozi walioagwa walitoa shukrani zao kwa uongozi wa Mahakama Kuu, watumishi na wadau mbalimbali waliojitokeza kuwaandalia na kushiriki hafla hiyo kwa pamoja na kuwapa zawadi malimbali nzuri ambazo walikiri kufurahishwa nazo katika tukio hilo.

Kwa niaba ya viongozi walioagwa, akitoa neno hilo la shukurani Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Songea Mhe. James Karayemaha aliwaahidi watumishi na wadau kuendelea kutoa ushirikiano kwa pamoja watendelea kuwa sehemu ya familia ya Kanda ya Mbeya na kutoa msaada wa kiutendaji wakati wowote watakapo itajika kufanya hivyo.

Katika tukio jingine, Mhe. Ndunguru alizindua klabu ya mazoezi ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ijulikanayo kama Mahakama Mbeya Jogging Club na kwa kutambua ushiriki wa viongozi walioagwa wakati klabu hiyo ilipoanzishwa.

Mhe. Ndunguru alitumia muda huo kuwagawia vifaa vya mazoezi kama vile Jezi viongozi walioagwa pamoja na watumishi wengine wa Mahakama ambao wamekuwa wakishiriki katika mazoezi hayo mara kwa mara. Mazoezi hayo yanyobeba kaulimbiu ijulikanayo kama Mazoezi ni Uchumi, Afya na Ndoa na kuwahimiza watumishi wote wa Mahakama kujiunga na klabu hiyo.

Hafla hiyo iliambatana na ugawaji wa tuzo na zawadi mbalimbali kwa viongozi walioagwa pamoja na watumishi wa Mahakama na wadu wa Mahakama (souvenir) kwa  kufanisha hafla hiyo.

Naye, Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu alitoa neno la shukurani kwa niaba ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kwa waalikwa kwa kuhudhulia kwao kwani walionesha upendo na umoja zaidi na aliendelea kusisitiza umoja na ushirikiano sehemu za kazi.


Sehemu ya Viongozi wa Mahakama waliohama Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya wakiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi wengine waliohamia Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya walipokuwa kwenye Mchaparo hafla hiyo ulifanyika tarehe 31 Mei, 2024 katika ukumbi wa Beaco Resort Kadege Mbeya. 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru akiongoza hafla hiyo mwanana.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Songea Mhe. James Karayemaha akitoa neno wakati wa hafla hiyo

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti akifurahia zawadi aliyokabidhiwa wakati wa hafla hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru akionyesha jezi za mazoezi zinazotumiwa na klabu ya mazoezi ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ijulikanayo kama Mahakama Mbeya Jogging Club, kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni