Jumanne, 9 Julai 2024

DC ARUMERU ASISITIZA USHIRIKIANO KUZIENDESHA KAMATI ZA MAADILI

 Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Arusha

Mkuu wa wilaya ya Arumeru na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilayani humo, Mhandisi Emmanuela Kaganda amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya Mihimili ya Dola ili kuwezesha wananchi kupata haki kwa wakati.  

Akizungumza wakati wa Utoaji wa Elimu kwa wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya Wilaya hiyo jana tarehe 8 Julai, 2024, Mkuu huyo wa wilaya alisema ushirikiano kati ya Mahakama na Serikali ni muhimu kwa kuwa Mihimili yote inalenga kumstawisha Mwananchi wa Tanzania.

“Natambua umuhimu wa Mahakama na ushirikiano unaohitajika kwani bila ushirikiano kati ya mihimili ya Dola, Mwananchi hatapata haki kwa wakati”, alisema.

Aidha, Mhandisi Kaganda ameihakikishia Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa Kamati anayoiongoza itafanya vikao vyake vilivyopangwa kwa mujibu wa Sheria. Vikao hivyo hutakiwa kufanyika mara nne kwa mwaka.

Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya Kamati, Mkuu huyo wa wilaya alisema Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Arumeru itatekeleza vema jukumu lake la kusimamia Maadili ya Mahakimu kwa kufuata kanuni, mwongozo na taratibu zilizowekwa ili kutenda haki.

Mkuu huyo wa Wilaya pia aliwashukuru Watumishi wa Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuona umuhimu wa kufika wilayani Arumeru na kutoa elimu kuhusu uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kwa wajumbe wa Kamati hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Alex Mbuya alisisitiza umuhimu wa wajumbe wa Kamati kula viapo kabla ya kuanza kushughulikia mashauri ya kinidhamu na kukabidhiana nyaraka muhimu zinazotumika katika kutekeleza kazi za Kamati za Maadili pale inapotokea uhamisho ili kuwe na muendelezo wa utekelezaji wa majukumu ya Kamati hizo.

Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya inaundwa na wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Katibu Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

Mkuu wa wilaya ya Arumeru na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilayani humo, Mhandisi Emmanuela Kaganda akifuatilia Mada wakati wa Utoaji wa Elimu kwa Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilaya ya Arumeru jana. Watumishi wa Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wananendelea na kazi ya Utoaji Elimu kwa Kamati hizo katika Mikoa ya Manyara na Arusha pamoja na wilaya zake.

Mkuu wa wilaya ya Arumeru na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilayani humo, Mhandisi Emmanuela Kaganda (Wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilaya ya Arumeru jana. Wa pili kushoto ni Naibu Katibu wa Tume (Nidhamu na Maadili) Bi. Alesia Mbuya.

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni