Jumanne, 9 Julai 2024

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA ASHANGAZWA NA MWAMKO MAONESHO SABASABA

  • Apongeza maandalizi yaliyofanyika
  • Akunwa na uwekezaji katika Taasisi shiriki

Na FAUSTINE KAPAMA -Mahakama, Dar es Salaam

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 9 Julai, 2024 ametembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa 2024, maarufu Sabasaba, kujionea shughuli mbalimbali za uwekezaji zinazofanywa na Wananchi na Taasisi mbalimbali.

Prof. Ole Gabriel aliwasili katika Viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke katika Mkoa wa Dar es Salaam majira ya saa 5.30 asubuhi na kukutana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Suleiman Jaffo katika Ofisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania.

Baada ya kupokea taarifa fupi kuhusu maonesho hayo, Mtendaji Mkuu alipitishwa katika mabanda mbalimbali aliyopangiwa ambayo ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi Moyo ya Jakaya Kikwete na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.

Mabanda mengine aliyotembelea ni Mifuko ya Jamii ya NSSSF na PSSSF, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mifugo, Mahakama ya Tanzania na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda hayo, Prof. Ole Gabriel amewapongeza waandaaji wa maonesho hayo ambayo yalifunguliwa na Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi, akiwa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kwa kweli maandalizi ni makubwa na yemefana. Sikuweza kutembelea mabanda yote, lakini nimeona mwamko mkubwa sana kwenye yale niliyotembelea. Bahati nzuri miaka ya nyuma ya 2001 hadi 2011 nilifanikiwa kuwa mmoja wa Majaji wa Maonesho kama haya. Niliyokuwa nayaona wakati ule na ninayoyaona sasa miaka hii ni mabadiliko makubwa sana,” amesema.

Mtendaji Mkuu ametoa mfano katika banda la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili namna uwekezaji mkubwa ulivyofanyika kwenye matibabu ambapo wamefikia katika hatua ya utalii wa kimatibabu, hivyo akampongeza Mkurugenzi Mkuu Prof. Mohamed Janabi na Watalaam Bingwa aliowakuta kwa kufanya mambo makubwa.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali yanayoshairisha maendeleo ya nchi na Watanzania kwa ujumla. Pia ametoa ushawishi kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kuendelea kuyapa uzito maonesho hayo kwani yameshavuka mipaka ya Tanzania na ni eneo ambalo watu wanaweza kujitangaza vizuri.

“Kuwa na bidhaa ni jambo moja, lakini kuhakikisha kwamba bidhaa ile imefahamika vizuri kwa jamii na kwenye soko ni jambo la muhimu zaidi. Ndiyo maana kwenye taaluma ya biashara kuna kitu kinaitwa marketing mix na moja wapo ni promotion. Maonesho haya ni moja ya promotion,” amesema.

Mtendaji Mkuu amewashauri Watanzania kutumia fursa hiyo vizuri siyo tu kuleta kwenye maonesho kuonyesha bidhaa, lakini ubora ni wa muhimu zaidi ili wateja wa ndani na nje waweze kuamini kwamba bidhaa iliyotengenezwa na Watanzania ni bora zaidi.

Amebainisha kuwa mara zote katika huduma au biashara mteja hanunui bidhaa, bali hununua thamani, hivyo ubora katika bidhaa husaidia kuongeza pato la Taifa, hasa pale kila mmoja anapotamani kuuza nje na kuwezesha kupata fedha nyingi za kigeni.

“Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametutengenezea mazingira mazuri ya diplomasia uchumi nje ya nchi, lililopo kwetu sisi ni kutumia fursa hii vizuri,” amesema.

Mahakama ya Tanzania imeweka kambi katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’, 2024 yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa huduma na elimu kwenye masuala mbalimbali ya Mahakama na sheria kwa ujumla.

Kwa mwaka huu, Viongozi na watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau mbalimbali ambao ni watalaam na wabobezi katika masuala ya kisheria wanaendelea kutoa huduma na elimu hiyo kwa muda wote wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’ ambayo yameanza tangu tarehe 28 Juni, 2024.

Katika kipindi chote cha Maonesho hayo, Mahakama inatoa huduma mbalimbali zikiwemo za kusikiliza Mashauri kwenye Mahakama Inayotembea ‘Mobile Court Services’, kutoa Msaada wa Kisheria ‘TLS’, elimu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani na safari ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasili katika Viwanja vya Sabasaba.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika banda la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika banda la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa mtumishi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasalimia wananchi waliokuwa wanapata huduma katika banda la Mfuko wa Jamii wa PSSSF.

 
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiongozwa kuelekea kwenye mabanda mengine.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisaini kwenye kitabu cha wageni katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria. Picha chini akiteta jambo na Katibu Mkuu, Bi. Mary Makondo.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akiingia katika banda la Mahakama ya Tanzania akiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi kwa upande wa Mahakama, Mhe. Hussein Mushi (aliyetangulia mbele).

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabrielakiwa katika banda la Usuluhishi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika banda la Idara ya Kumbukumbu na Huduma za Maktaba.

 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa ndani ya Mahakama Inayotembea.
(Picha na JEREMIA LUBANGO)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni