Jumanne, 16 Julai 2024

JAJI MFAWIDHI SONGEA ARIDHIA KUANZA HUDUMA ZA KIMAHAKAMA MAGAZINI, NAMASAKATA

Na NOEL SYLIVESTER – Mahakama, Songea

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha hivi karibuni alifanya ziara ya kimahakama katika Wilaya za Namtumbo na Tunduru na kuridhia huduma za Mahakama za Mwanzo kuanza kutolewa katika Vijiji vya Magazini na Namasakata kuanzia mwezi Agosti, 2024.

Hata hivyo, Mhe. Karayemaha hakuridhia huduma za Mahakama za Mwanzo katika Kijiji cha Lukumbule kuanza kutolewa kwa sasa baada ya kutoridhishwa na jengo ambalo limetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo kutokidhi vigezo vinavyotakiwa kwa ajili ya utoaji huduma za kimahakama.

Jaji Mfawidhi alianza ziara yake kwa kutembelea Kijiji cha Magazini kilichopo katika Wilaya ya Namtumbo inapopatikana Mahakama ya Mwanzo Magazini. Serikali ya Kijiji ilishukuru kwa ujio wake kwa sababu ni Jaji wa kwanza kutembelea eneo hilo.

Wanakijiji hao walijitolea jengo litakalotumika katika utoaji wa huduma za kimahakama katika Kijiji cha Magazini. Kutokana na jitihada hizo, Jaji Mfawidhi akatoa kibali cha kuanzishwa huduma za Mahakama za Mwanzo mwishoni mwa mwezi Agosti 2024 baada ya marekebisho madogo madogo kukamilika.

Vile vile, Mhe. Karayemaha alitembelea maeneo katika Kijiji cha Lukumbule iliyopo Wilaya ya Tunduru ambayo Serikali ya Kijiji iliyaainisha kama yanaweza kutumika kwa kutolea huduma za kimahakama.

Hata hivyo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. Elizabeth Nyembere na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Epaphras Tendanamba, wakaona maeneo hayo hayajakidhi vigezo vinavyotakiwa kwa ajili ya utoaji huduma za kimahakama.

Hivyo ikashauriwa wananchi wa eneo hilo wajitolee kuchangia ujenzi wa jengo jipya ili huduma za kimahakama zirejeshwe ndani ya mwaka huu 2024 kwa sababu huduma za Mahakama za Mwanzo zimesimama tangia mwaka1990.

Akiwa katika Kijiji cha Namasakata kilichopo Wilaya ya Tunduru na inapopatikana Mahakama ya Mwanzo Namasakata, Mhe. Karayemaha alipokea taarifa ya historia ya utoaji wa huduma za kimahakama kutoka kwa mjumbe wa Serikali ya Kijiji.

“Mimi ninavyofahamu katika kukua kwangu, huduma ya Mahakama hapa Namasakata ilikuwa inatolewa kipindi cha mkoloni na baada ya uhuru hadi mwaka 1985 jengo lilipoanguka,” alisema mjumbe huyo.

Jaji Mfawidhi alielezwa kuwa kutokana na kukosekana kwa Mahakama hiyo wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakifuata huduma za kimahakama katika Mahakama ya Mwanzo Mlingoti iliopo Tunduru mjini, hivyo kukosa haki zao za msingi kutokana na umbali usiopungua kilomita 70. 

Baada ya kuridhishwa na jengo lililotolewa na uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Namasakata, Mhe. Karayemaha alitoa kibali cha kurejesha huduma za kimahakama kuanzia tarehe 01 Agosti, 2024. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (kulia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Simon Kamori Chacha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (wa kwanza kushoto) akiwa sambamba na Mtendaji wa Mahakama Songea, Bw. Epaphras Tenganamba (wa pili kutoka kushoto) wakikagua kiwanja cha Mahakama ya Mwanzo Lukumbule.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (aliyevaa kaunda suti nyeusi) akisalimiana na uongozi wa Serilkali ya Kijiji Magazini.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (wa nne kutoka kushoto) na Naibu Msajili, Mhe. Elizabeth Nyembere (wa kwanza kutoka kulia) wakiwa na uongozi wa Serikali ya Kijiji Namasakata  (waliopo nyuma).

Uongozi wa Serikali ya Kijiji Namasakata ukiwa kwenye kikao baada ya kumpokea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha. 

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni