Jumanne, 16 Julai 2024

‘SITAWAANGUSHA TUTAENDELEA KUCHAPA KAZI’ – JAJI MUGETA

  • Ataja vipaumbele vinne vya kusimamia kazi

Na SETH KAZIMOTO-Mahakama, Arusha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta amewaahidi watumishi wa Mahakama mkoani Arusha kuwa hatawaangusha katika kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake, Mhe. Joachim Tiganga ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kuwa Jaji Mfawidhi.

Mhe. Mugeta aliyasema hayo jana tarehe 15 Julai, 2024 katika hafla fupi ya kumpokea iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama waliohudhuria katika hafla hiyo, Mhe. Mugeta alitaja vipaumbele vyake atakavyosimamia katika utendaji kazi kuwa ni pamoja na nidhamu ya kazi na maadili, usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa mashauri ya mirathi, kusikiliza na kumaliza mashauri kwa wakati na utoaji elimu kwa watumishi na wateja wa Mahakama.

Awali, aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Mhe. Tiganga alimkaribisha Mhe. Mugeta na kumueleza kuwa, watumishi wa Mahakama mkoani Arusha ni wachapa kazi na hodari ambao wako tayari kutoa ushirikiano wao kwa kiongozi.

‘‘Naomba muendelee kutoa ushirikiano kwa Jaji Mugeta kama mlivyokuwa mnafanya kwangu ili shughuli za Mahakama ziendelee kwa ufanisi zaidi,’’ alisisitiza Mhe. Tiganga.

Kabla ya kuhamishiwa Kanda ya Arusha, Jaji Mugeta alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa na aliyekuwa Jaji Mfawidhi Mahakama wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Tiganga amehamishiwa Mbeya kuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo.

Hafla hiyo fupi ilihudhuriwa na Majaji wa Mahakama hiyo, Naibu Msajili, Mtendaji, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Arusha na Arumeru, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo Arusha Mjini na Themi pamoja na watumishi wa Mahakama mkoani humo.


Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga (kulia) akimkaribisha Mhe. Ilvin Mugeta mara baada ya kuripoti Mahakama Kuu Arusha jana tarehe 15 Julai, 2024 tayari kwa kuanza kazi. Mhe. Tiganga amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kuwa Jaji Mfwidhi wa Kanda hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba (kulia) akimkabidhi ua Jaji Mfawidhi mpya wa Kanda ya Arusha, Mhe.Ilvin Mugeta alipowasili katika viunga vya Mahakama Kuu Arusha jana tarehe 15 Julai, 2024. Wanaoshuhudia upande wa kulia ni Majaji wa Mahakama hiyo.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga (kushoto) akikabidhi Ofisi kwa Mhe. Ilvin Mugeta ambaye aliripoti jana tarehe 15 Julai, 2024.

Jaji Ilvin Mugeta (kushoto) na Joachim Tiganga (kulia) wakikata keki kwa pamoja kama ishara ya umoja na upendo wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha Mhe. Mugeta iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha jana tarehe 15 Julai, 2024.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya (aliyesimama) akitoa neno la shukrani wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha Mhe. Ilvin Mugeta iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha jana tarehe 15 Julai, 2024.

(Habari hii imehaririwa MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni