Ijumaa, 5 Julai 2024

JAJI MKUU ATEMBELEA MAONESHO YA SABASABA

  • Asema Tanzania mahala sahihi kuwekeza, kufanya biashara

Na Faustine Kapama-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 5 Julai, 2024 ametembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa 2024, maarufu Sabasaba, ili kujionea shughuli mbalimbali za uwekezaji na kiuchumi zinazofanywa na wananchi na Makampuni kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Mhe. Prof. Juma aliwasili katika Viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke katika Mkoa wa Dar es Salaam majira ya saa 5.00 asubuhi na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania na Mahakama.

Jaji Mkuu aliambatana na Viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Victor Kategere, Katibu wa Jaji Mkuu na Naibu Msajili, Mhe. Venance Mlingi na wengine.

Baada ya kupokea taarifa fupi kuhusu maonesho hayo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Bi. Ratifa Khamis, Jaji Mkuu alipitishwa katika Mabanda mbalimbali ambayo yalionekana kufurika wananchi.

Mhe. Prof. Juma aliongozwa na Mamlaka kutembelea mabanda tisa, ikiwemo Shirika la Bima la Taifa, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Wizara ya Viwanda na Biashara, Mahakama ya Tanzania, Magereza, Ofisi ya Waziri Mkuu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kutembelea Mabanda hayo, Jaji Mkuu amethibitisha ile Kauli Mbiu ya Maonesho ya 48, kwamba Tanzania ni mahala sahihi pa kufanya biashara na uwekezaji.

“Katika maeneo machache ambayo nimepata nafasi ya kuyatembelea nimeweza kuona uwekezaji mkubwa sana, hasa katika maeneo ambayo yatakuwa chachu kwa sekta binafsi kuweza kukua na kuendelea,” amesema.

Jaji Mkuu amebainisha kuwa yapo maeneo ambayo uwekezaji utasaidia huduma za biashara kuweza kufanyika, hivyo maonesho hayo yanatoa picha ya Tanzania ya sasa na ile inayokuja.

Amesema pia kuwa kuna maeneo mengine ambayo yanaweza kusaidia, hasa katika uwekezaji na biashara na kupunguza milolongo ya kutoa maamuzi. 

“Siku hizi kuna dhana ya mchakato wa biashara (business process), tunaifanyia mchakato upya. Badala ya mchakato wa kibiashara kupitia hatua 10 au 20, tukiweza kuzipunguza kuwa hatua mbili au tatu, Tanzania itakuwa eneo bora la uwekezaji na biashara,” amesema.

Akizunguzia Banda la Mahakama, Mhe. Prof. Juma ameona uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali kama miundombinu ya majengo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na uwekezaji katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa na malalamiko yao yanafanyiwa kazi.

“Mahakamani kuna maboresho makubwa katika huduma, tumefikia hatua ya kutoa huduma ya Mahakama Inayotembea. Mahakama ni mfano katika matumizi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao unatumika pia katika kutoa haki…

“Wito wangu ni kwamba huduma za mtandao kadri zinavyosogezwa vijijini, hivyo hivyo huduma za Mahakama ndiyo zitazidi kusongea karibu na wananchi. Kwa hiyo ni uwekezaji mkubwa nimeuona,” Jaji Mkuu amesema.

Kabla ya Jaji Mkuu kuwasili katika Viwanja vya Sabasaba, Banda la Mahakama lilitembelewa na Majaji wa tatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe. Cyprian Phocas Mkeha, ambaye ni Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Ubena John Agatho, Mhe. Dkt. Cleophace Morris na Mhe. Abdallah Halfan Gonzi.

Viongozi wengine waliotembelea banda la Mahakama ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas James Lyimo na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Wakili Msomi Harold Sungusia.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokelewa kwenye Viwanja vya Sabasaba na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, Bi. Ratifa Khamis. Picha chini akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Ofisi za Mamlaka hiyo.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akisikiliza maelezo mafupi kuhusu maonesho hayo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, Bi. Ratifa Khamis. 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) katika picha ya pamoja

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongozwa kuelekea kwenye mabanda mbalimbali.
 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika Banda la Ofisi ya Waziri Mkuu. Picha chini akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali kutoka ofisi hiyo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ndani ya banda la Magereza (juu na chini).



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipata maelezo katika banda la Mahakama ya Tanzania kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu maonesho hayo kwa épande wa Mahakama, Mhe. Hussein Mushi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na Lucky Eunice Michael katika banda la maboresho/ usimamizi wa majengo.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika banda la huduma bora kwa mteja.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika banda la usuluhishi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania wanaoshiriki kwenye maonesho ya Sabasaba.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikaribishwa kwenye banda la Wizara ya Uchukuzi.






Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea zawadi kutoka kwa Mmoja wa watumishi wa Wizara hiyo.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea zawadi baada ya kutembelea banda la Shirika la Mawasiliano (TTCL). Picha chini akipata maelezo kadhaa.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja baada ya kutembelea banda la Bandari. Picha chini akikabidhiwa zawadi.




Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa ndani ya banda la Shirika la Bima Tanzania (picha mbili juu). Picha chini akikabidhiwa zawadi.




Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akizungumza na Waandishi wa Habari.


Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara wakipata elimu kwenye banda la Mahakama ya Afrika Mashariki. Kutoka kushoto kuanzia wa pili ni Mhe. Cyprian Phocas Mkeha , ambaye ni Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Cleophace Morris, Mhe. Abdallah Halfan Gonzi na Mhe. Dkt. Ubena John Agatho.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara wakipata elimu kwenye banda la Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi. Kutoka kulia ni Mhe. Cyprian Phocas Mkeha, ambaye ni Jaji Mfawidhi, Mhe. Abdallah Halfan Gonzi, Mhe. Dkt. Cleophace Morris na Mhe. Dkt. Ubena John Agatho.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni