Ijumaa, 5 Julai 2024

WAFUNGWA NA MAHABUSU WAIPONGEZA MAHAKAMA KWA KUTATUA KERO ZAO

 

Na. Francisca Swai, Mahakama – Musoma.

Wafungwa na mahabusu wa Gereza Musoma wameipongeza Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma kwa kusikiliza na kutatua kero zao mbalimbali hasa zinazohusiana na mashauri. 

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ukaguzi wa gereza hilo uliofanywa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya, hivi karibuni akiambatana na wadau mbalimbali wa Mahakama. 

Aidha wafungwa wa Gereza hilo wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuongeza vikao vya Mahakama ya Rufani vinavyokaa Musoma ili kusikiliza mashauri yao kuwa vinne kwa mwaka, tofauti na ilivyokuwa hapo awali walikuwa wakija mara mbili kwa mwaka. Hatua hiyo itasaidia mashauri yao kusikilizwa kwa haraka na kupata haki zao kwa wakati.

Pamoja na pongezi hizo, wafungwa na mahabusu hao wameiomba Mahakama pamoja na wadau wake kuongeza vipindi vya utoaji elimu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria kwao.

‘‘Mahakama na wadau wake hutoa elimu wakati wa wiki ya sheria na siku wanapokuja kwa ajili ya ukaguzi wa gereza, ila tunaomba vipindi vya elimu viongezwe ili tupate uelewa zaidi utakaotusaidia katika mashauri yetu na hata tutakapotoka gerezani tukawe raia wema,’’ alisema mmoja wa wafungwa aliyeko gereza Musoma.

Akipokea pongezi hizo, Mhe.  Mtulya  amewasisitiza wafungwa na mahabusu hao kuendelea kuzoea matumizi ya TEHAMA hasa pale mashauri yao yanaposikilizwa kwa njia ya video (Video Conference). 

Alisema njia hiyo ya video inarahisisha usikilizwaji wa mashauri yao na kuwa kwa njia hiyo yanamalizika kwa wakati na kupunguza adha za kutokufika mahakamani kwa wakati jambo linalosababisha kuahirishwa kwa mashauri yao hivyo kukaa gerezani kwa muda mrefu.

Sambamba na ukaguzi wa gereza hilo,  Mhe. Fahamu Mtulya, amefanya ukaguzi wa mahakama mbalimbali katika Wilaya za Butiama na Bunda.

Katika ukaguzi huo, Mhe. Mtulya aliongozana na viongozi mbalimbali wa Kanda ya Musoma, ambapo aliwaasa watumishi kuendelea kujiimarisha vema katika matumizi ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na kusikiliza mashauri kwa njia ya video, kuendelea kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na maadili.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi, wamewapongeza watumishi kwa kazi nzuri na kuwaasa kuishi kwa upendo na umoja.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Gereza Musoma, SSP, J. Murya (kushoto kwa Mhe. Jaji Mfawidhi) pamoja na wadau mbalimbali wa Mahakama walioshirikiana katika kutoa elimu na ukaguzi wa gereza Musoma.


Mlinzi wa Mahakama ya Mwanzo Zanaki iliyoko Wilayani Butiama Bw. Albinus Simeo (aliyenyoosha mkono) akimuonesha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kushoto) pamoja na viongozi wengine mipaka ya eneo la Mahakama hiyo.

 Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Butiama Bi. Teckla Patrick (aliyesimama) akifafanua jambo kwa viongozi wakati wa ukaguzi uliofanywa katika Mahakama hiyo.

Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi, wa Mahakama ya Wilaya Butiama, Mhe. Chiza Kabwebwe (aliyesimama) akitoa maelezo  mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (aliyekaa) wakati wa ukaguzi uliofanywa katika Mahakama hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (wa kwanza kulia) akitoa maelekezo wakati wa ukaguzi wa Mahakama ya Mwanzo Kabasa iliyoko Wilayani Bunda.

Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi, wa Mahakama ya Wilaya Bunda, Mhe. Betron Sokanya (aliyesimama) akisoma taarifa ya utekelezaji na utendaji kazi wa Mahakama ya Wilaya Bunda mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (aliyekaa mbele) wakati wa ukaguzi uliofanywa katika Mahakama hiyo.
 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (katikati mbele), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha (wa pili kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi (wa kwanza kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Bunda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni