Jumamosi, 6 Julai 2024

JAJI MTULYA AWAPIGA MSASA WANAFUNZI WA MWEKA

 Na. FRANCISCA  SWAI, Mahakama – Musoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amewaasa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori (MWEKA) kuzingatia masomo yao ili baadae waweze kulitumikia taifa kwa kulinda maliasili iliyopo kwa weledi na uaminifu.

Akiwa katika ziara yake ya ukaguzi wa Mahakama Wilayani Serengeti hivi karibuni Mhe.Jaji Mtulya, alikutana na jumla ya wanafunzi 120 wa mwaka wa pili, wanaosomea Shahada ya kwanza ya Uhifadhi wa Wanyamapori kutoka katika chuo hicho. 

Wanafunzi hao wako kwenye ziara ya siku mbili katika Mahakama ya Wilaya Serengeti ambapo wanajifunza kwa vitendo juu ya taratibu za Mahakama katika uendeshaji wa mashauri ya nyara.

Akizungumza na wanafunzi hao, Mhe. Mtulya aliwaasa kuzingatia masomo yao ili baadae walitumikie taifa katika sekta ya utalii na uhifadhi wa wanyama pori ambayo ni muhimu katika kuliingizia taifa mapato lakini pia ikiwa ni njia ya wao kupata vipato vyao halali.

‘‘Kwa namna kazi zenu zilivyo, jiepusheni sana na mkumbo wa kuingia kwenye makundi ya watu wasio waaminifu wanaohusika na biashara haramu za kusafirisha wanyama na mali asili za taifa. Someni kwa bidii ili muulinde urithi wa nchi yetu kwa manufaa yetu na ya vizazi vijavyo,’’alisema Mhe. Jaji Mtulya.

Aidha, amewaeleza wanafunzi hao namna bora ya kushughulikia mashauri ya nyara pamoja na maeneo muhimu ya kuzingatia ili kuthibitisha mashauri hayo Mahakamani kwa lengo la kukomesha uvamizi wa maeneo ya hifadhi na uwindaji haramu wa wanyama pori. Pia amewaelezea kwa undani uhusinao uliopo kati ya Polisi, Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali na Mahakama katika usikilizwaji wa mashauri hayo.

Naye Mwalimu Khalfan Kiondo aliyeongozana na wanafunzi hao kutoka katika chuo hicho aliushukuru uongozi wa Mahakama Kanda ya Musoma kwani muda wote wamekuwa wakipata ushirikiano wa kutosha kutoka katika mahakama mbalimbali za kanda hiyo kwa ajili ya mafunzo ya wanafunzi hao.

Katika ziara hiyo Jaji Mtulya alioongozana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi katika kufanya ukaguzi wa Mahakama Wilayani Serengeti na Tarime.

Viongozi hao walipata nafasi ya kuongea na watumishi, kutatua changamoto mbalimbali walizokutana nazo na kusisitiza usikilizwaji wa mashauri kwa wakati, matumizi ya TEHAMA, ulinzi wa mipaka, kufanya kazi kwa uaminifu, weledi na uwajibikaji. 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Serengeti wakati wa ukaguzi alioufanya katika Mahakama hiyo.

Ja ji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (katikati mbele), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha (wa pili kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Serengeti.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (aliyesimama katikati), akizungumza na wanafunzi na walimu kutoka katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori (MWEKA) walioko Wilayani Serengeti kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Wa tatu kushoto(mwenye tisheti nyekundu) ni mwalimu Khalfani Kiondo aliyeambatana na wanafunzi hao kutoka katika chuo hicho.

Mwanafunzi wa mwaka wa pili kutoka katika chuo hicho Bw. Elias Chacha (aliyesimama katikati) akiuliza swali kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (aliyesimama mbele).

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kenyana iliyoko Wilayani Serengeti Mhe. Peter Malima (aliyenyoosha mkono) akielezea jambo kuhusu mipaka ya eneo la Mahakama hiyo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (wa tatu kushoto) pamoja na viongozi wengine waliotembelea Mahakama hiyo kwa ukaguzi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiwa katik apicha ya pamoja na viongozi na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Ngoreme iliyoko Wilayani Serengeti wakati wa ukaguzi uliofanywa katika Mahakama hiyo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Nyamwigura Mhe. Boniface Mhuza (aliyesimama) akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni