Jumamosi, 6 Julai 2024

JAJI NKWABI AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA HUDUMA ZA MAHAKAMA UVINZA

Akagua pia ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Uvinza

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi, tarehe 4, Julai 2024 amefanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za kimahakama na kiutawala Mahakama ya Wilaya ya Uvinza sambamba na kukagua ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Uvinza unaoendelea kwa kwa kutumia fedha za matumizi ya kawaida.

Akizungumza na Watendaji wa Mahakama hiyo tarehe 04 Julai, 2024 kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Kigoma, Mhe. Nkwabi aliwasisitiza Watendaji kusimamia ipasavyo ujenzi huo na kuhakikisha unakamilika kabla ama ifikapo tarehe 30 Julai, 2024 ili shughuli za kimahakama zirejee ifikapo tarehe 01 Agosti, 2024. 

“Kukamilika kwa ujenzi huu kutawapunguzia wananchi kero kwani walikuwa wakisafiri umbali mrefu kilomita 22 kufuata huduma ya haki,” alisema Mhe. Nkwabi. 

Ujenzi wa jengo hilo jipya ulianza baada ya jengo la awali kudondoka kutokana na uchakavu. 

Akitoa taarifa ya ujenzi huo, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay alieleza kuwa, kukamilika kwa jengo hilo kutarahisisha utoaji wa huduma za Mahakama na kutoa haki kwa wakati kama inavyoainishwa katika Dira ya Mahakama ya kuhudumia wananchi bila kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Aliendelea kueleza kwamba, jengo hilo lenye vyumba viwili, mapokezi na choo linalojengwa kwa siku 60 kwa kutumia utaratibu wa ‘force account’ utagharimu kiasi cha fedha kisichozidi milioni 30. 

“Iwapo ujenzi huu ungetumia utaratibu wa zabuni ungegharamu zaidi ya shilingi milioni 50,” alisema Bw. Matotay.

Katika hatua nyingine, Jaji Nkwabi aliwapongeza watumishi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza pamoja na uchache wao kwa kufikia malengo waliyojiwekea kwani kila mtumishi anatekeleza jukumu zaidi ya moja kama inavyosisitizwa na Uongozi wa Mahakama katika kuongeza ufanisi wa shuguli za kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, Mhe. Frank Mtega, akitoa taarifa ya utendaji wa Mahakama hiyo,  alisema kuwa inasimamia Mahakama moja ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo tano. 

Aidha, Mhe. Mtega aliendelea kueleza kuwa, Mahakama hiyo kwa sasa inaendesha shughuli za kimahakama na utawala kidigiti na katika kipindi cha mwezi Aprili – Juni, 2024 imesajili jumla ya mashauri 51 kwa njia ya mtandao na mashauri 80 yamesikilizwa kwa njia ya mtandao. 

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi (kushoto) akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Uvinza mara baada ya kuwasili mahakamani hapo tarehe 04 Julai, 2024 kwa ajili ya ziara ya ukaguzi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza pamoja na Viongozi alioambatana nao kutoka Mahakama Kuu Kigoma.  Wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma,  Bw. Filbert Matotay, wa pili kulia ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama Wilaya Uvinza, Mhe. Frank Mtega akifuatiwa na Afisa Tawala wa Mahakama hiyo, Bw. Tumaini. 

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma,  Bw. Filbert Matotay (kushoto) akifafanua jambo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Francis Nkwabi wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Uvinza. 

 Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza, Mhe. Frank Mtega akitoa taarifa ya utendaji kwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma,  Mhe. Francis Nkwabi (hayupo katika picha).
Picha ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Uvinza linaloendelea kujengwa kwa ajili ya kurejesha huduma za Mahakama hiyo zilizohamishiwa kwenye jengo la Mahakama ya Wilaya Uvinza.

Picha ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Uvinza lililofungwa baada ya  kuonyesha dalili za uchakavu ikiwemo nyufa kubwa katika pande zote za jengo hilo zilizosababisha kufungwa kwa huduma za Mahakama katika jengo hilo.

(Habari hii imehaririwa MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni