Na Abdallah Salum, Mahakama-Njombe
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama, Mhe. Dkt, Angelo Rumisha sanjari na ujumbe kutoka Benki ya Dunia wamemtaka Mkandarasi, Bw. Lee Manchao kutoka Kampuni ya Shadong inayosimamia ujenzi wa Kituo cha Utoaji Haki (IJC) Njombe kuongeza kasi ya ujenzi wa Kituo hicho ili kukamilisha kwa wakati waliokubaliana.
Agizo hilo lilitolewa jana tarehe 25 Julai, 2024 katika kikao cha pamoja na Mkandarasi huyo kilichohusisha ujumbe kutoka Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia walipofanya ziara ya ukaguzi wa Mradi wa ujenzi huo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Christine Owour alisema kuwa, Mradi huo unakwenda taratibu, hivyo, amewashauri Wahandisi waweze kujadiliana kufikia lengo ili Mradi huo uweze kumalizika kwa wakati.
Naye, Afisa Mwandamizi kutoka Benki ya Dunia, Bw. Benjamin Mtesigwa aliwashauri Wakandarasi kuwa na mpango kazi ili kufidia muda uliopotea.
Kwa upande wake Afisa Mazingira, Bi. Edina Kashangaki alifanya tathmini ya maendeleo ya ujenzi na kutoa pongezi kwa upande wa wafanyakazi kwamba hakuna unyanyasaji wa kijinsia, lakini pia alipitia mikataba ya wafanyakazi na kuangalia michango yao inaingia kwenye mfuko wa NSSF.
Aidha, Mkandarasi wa Mradi huo alitoa sababu ambazo zimechelewesha kuwa ni pamoja na hali ya hewa iliyochangiwa na mvua nyingi za masika kuanzia Januari-Aprili mwaka huu pamoja na vifaa kucheleweshwa kufika eneo husika.
Mradi wa Ujenzi wa IJC Njombe pamoja na Vituo vingine nane vinavyoendelea kujengwa nchini unafadhiliwa na fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Mhandisi ujenzi IJC Njombe, Bw.Harold Ngumuo (kushoto) akiwaonesha wajumbe kutoka Mahakama na Benki ya Dunia jinsi ramani ya Kituo hicho ilivyokaa na ujenzi unavyoendelea jana tarehe 25 Julai, 2024. Kutoka kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha anayefuata Kiongozi wa Msafara kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owour na aliyesimama kushoto kwa Mhandisi Afisa Mazingira, Bi. Edina Kashangaki pamoja na Wakandarasi wengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni