Alhamisi, 25 Julai 2024

USHIRIKIANO WA TUME NA CHUO CHA MAHAKAMA UTAIMARISHA UTOAJI HAKI

 ·       Tume kuendelea kusimamia suala la kuwajengea uwezo Watumishi wa  Mahakama

Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Lushoto-Tanga

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira amesema Ushirikiano Kati ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na chuo hicho utaiwezesha Mahakama ya Tanzania kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kikatiba ka kutoa haki kwa wananchi.

Akizungumza na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama waliofanya ziara kwenye chuo hicho jana, Jaji Levira alisema ushirikiano kati ya Tume na Chuo cha Uongozi wa Mahakama utaleta matokeo chanya katika kuimarisha utendaji kazi wa Mahakama kwa kuwa chuo hicho hutoa mafunzo ya kimahakama kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania.

”Tunawashukuru kwa kufika chuoni hapa na kuzungumza nasi, mazungumzo haya ni moja ya mikakati ya kusaidia kuendeleza malengo ya Chuo hiki, Tume pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa ujumla” , alisema.

 Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Ajira) Bi. Enziel Mtei amesema Tume itaendelea kusimamia suala la kuwajengea uwezo Maafisa Mahakama pamoja na watumishi wasio Maafisa Mahakama ili kuiwezesha Mahakama kutimiza lengo lake la kutoa huduma bora za haki.

”Tume ya Utumishi wa Mahakama ndiyo mamlaka ya ajira na uteuzi wa Viongozi mbalimbali wa Mahakama kwa mujibu wa sheria, ukiacha wale ambao mamlaka yao ya uteuzi ni Mhe. Rais,”alisema.

Alisema ili Mahakama iweze kutoa huduma bora na kwa ufanisi, inahitaji rasilimali bora na hili litawezekana kwa kuwa na watumishi wenye weledi wa kutosha, hivyo kuiwezesha Mahakama kutimiza matarajio yake ya kutoa huduma za haki kwa wakati na kwa ubora.

Akielezea ziara ya Makamishna chuoni hapo, Bi. Mtei alisema ni utaratibu wa Tume kuwa wanapoteuliwa Makamishna wapya hutembelea chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa lengo la kujifunza namna chuo kinavyotekeleza jukumu la kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama ya Tanzania.

Alisema mikakati inayotekelezwa na Tume ni kusimamia Mahakama na kuhakikisha kwamba watumishi wapya wanapoajiriwa wanapatiwa mafunzo elekezi kwa lengo la kuelewa Utumishi na misingi yake ikiwemo sera, kanuni na taratibu mbalimbali za utendaji kazi Serikalini, kufahamu majukumu yao na kuzingatia maadili, nidhamu, uadilifu na ustahimilifu.

Bi. Mtei alisema kuwa ni matarajio ya Tume kuwa mafunzo ya aina hiyo yanapofanyika, chuo kitakuwa na utaratibu wa kufanya tathmini kwa kila kundi na mshiriki moja moja, kuainisha mapungufu au ubora katika eneo lolote na kuwasilisha Taarifa hiyo Tume ili kuiwezesha kuboresha namna inavyotekeleza majukumu yake hasa kwenye eneo la ajira, upandishaji vyeo pamoja na uteuzi.

Katika ziara hiyo, Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama walipata nafasi ya kujifunza utendaji kazi wa chuo hicho kupitia mada iliyowasilishwa na Mkuu wa Chuo hicho, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul Kihwelo. Mada nyingine iliyotolewa ilihusu Muundo wa Mahakama ya Tanzania ambayo iliwasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga Mhe. Katarina Revokati Mteule.

Aidha, Makamishna walipata wasaa wa kuchangia mada hizo ambapo kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika alikishauri chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kuongeza msukumo wa kufundisha zaidi kwenye eneo la uandishi wa hukumu ili kuimarisha utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania.

Naye Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakili Bahame Tom Nyanduga alikishauri chuo hicho kuimarisha ufundishaji kwenye somo la Haki za Binadamu kwa lengo la kuwajenga na kuwaandaa Mahakimu na Waendesha Mashtaka kuzingatia haki za binadamu wanapotekeleza majukumu yao ya utoaji wa haki.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira akizungumza na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakati wa ziara yao kwenye Chuo hicho jana. 
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Ajira) Bi. Enziel Mtei nakizungumza wakati wa ziara hiyo.
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakifuatilia jambo wakati wa ziara yao katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto jana. 

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira akiongoza Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kutembelea majengo ya Chuo hicho.  

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kulia) akiwa na Viongozi wengine wa chuo hicho wakati wa ziara ya Makamishna wa Tume kwenye Chuo hicho jana. Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akielezea utendaji kazi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Katarina Revokati Mteule akielezea Muundo wa Mahakama ya Tanzania kwa Makamishna wa Tume wakati wa ziara yao kwenye Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto jana.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni