Alhamisi, 25 Julai 2024

MAHAKAMA YAANZISHA MFUMO MPYA WA UTOAJI HUDUMA KWA WATEJA

Walenga kuongeza ufanisi wa kuhudumia wateja

Una uwezo wa kuhudumia watu wengi kwa mkupuo

Na Jeremia Lubango, Mahakama-Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya ameipongeza Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya Mahakama kwa kuja na Mfumo mpya wa Utoaji Huduma kwa Wateja (Call Centre Application System) ambao unaenda kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama.

Akizungumza leo tarehe 25 Julai, 2024 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo elekezi kwa Maafisa wa Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Centre) cha Mahakama juu ya namna ya kuutumia mfumo huo, Mhe. Nkya amesema Mfumo huo utaweza kurekodi na kuhudumia wateja wengi zaidi kwa wakati mmoja.

“Dunia ya sasa inaongozwa na TEHAMA na dhamira ya Mahakama ni kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa kutumia TEHAMA, hivyo nipongeze ubunifu huu ambao utarahisisha utoaji huduma kwa wananchi,” amesema Msajili Mkuu.

Kadhalika, amezipongeza pia Kurugenzi ya Ukaguzi, Huduma za Mahakama na Maadili pamoja na Kurugenzi ya Mipango na Ufuatiliaji kwa jinsi wanavyosimamia utendaji kazi mzuri wa Kituo cha Huduma kwa Mteja ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za Mahakama.

Amesema, Mfumo huo ambao una uwezo wa kuhudumia watu wengi zaidi ndani ya dakika moja, utatoa ripoti ya siku, wiki, mwezi na mwaka na kuongeza kuwa, Mfumo huo unapatikana kwa kupiga namba ya bure ya 0800 750 247.

Ameongeza kwamba, anafahamu ipo mirejesho inayowahusu watumishi wenye vyeo mbalimbali kwenye Mhimili wa Mahakama ambapo amewasihi Maafisa wa Kituo hicho kufuatilia mirejesho hiyo kwa heshima na kuzingatia utu wa watumishi wengine bila hofu wala upendeleo lakini pia kuzingatia maadili, Katiba, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Mahakama.

Ametoa rai pia kwa watoa huduma kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuimarisha huduma. Amesisitiza hilo kwa kusema, “kushirikiana kutatua changamoto zinazowakabili kutasaidia kuongeza ufanisi mzuri wa ufanyaji kazi na kutachangia kuleta huduma bora na kuimarisha imani kwa wananchi na Mahakama kwa ujumla.”

Akizungumzia umuhimu wa Kituo hicho, Msajili Mkuu ameeleza kwamba, “Kituo cha Huduma kwa Mteja kimehusika katika ongezeko la kiwango cha kuridhika kwa watumiaji wa huduma za Mahakama kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na REPOA kutoka asilimia 78 kwa mwaka 2019 hadi asilimia 88 kwa mwaka 2023 kwa kutatua baadhi ya changamoto za wateja wa Mahakama na hivyo kupunguza malalamiko.”

Naye Mkurugenzi wa Ukaguzi, Huduma za Mahakama na Maadili wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Maira Kasonde amesema kwamba, Mfumo huo utaunganisha kurasa za Mahakama za mitandao ya kijamii ambazo ni ‘facebook’ (Mahakama ya Tanzania), ‘twitter’ (judiciarytz) na ‘instagram’ (judiciarytz) ambapo utasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mafunzo hayo ya siku nne yaliyoongozwa na Afisa na Msimamizi wa Mifumo ya TEHAMA, Mahakama ya Tanzania, Bw. Witness Ndenza pamoja na Bw. Mussa Ulekwe kutoka kampuni ya Utengenezaji wa Mifumo (MFI).

Mafunzo haya yalihudhuriwa na Viongozi kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi, Huduma za Mahakama na Maadili pamoja na Watumishi kutoka Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama.

Afisa na Msimamizi wa Mifumo ya TEHAMA, Mahakama ya Tanzania, Bw. Witness Ndenza (kushoto) akitoa maelezo kwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (wa tatu kushoto) leo tarehe 25 Julai, 2024 wakati alipotembelea chumba maalum cha Maafisa wanatoa huduma kwa wateja kilichopo ndani ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kulia kwa Msajili Mkuu ni Mkurugenzi wa Ukaguzi, Huduma za Mahakama na Maadili wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Maira Kasonde pamoja na Watumishi wengine wa Kituo hicho.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akizungumza wakati wa kufunga mafunzo elekezi mfumo mpya wa ushughulikiaji wa mirejesho kwa wateja yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 25 Julai, 2024.

Afisa na Msimamizi wa Mifumo ya TEHAMA, Mahakama ya Tanzania, Bw. Witness Ndenza (aliyesimama mbele) akitoa maelezo wakati wa ufungaji wa mafunzo elekezi ya mfumo mpya wa ushughulikiaji wa mirejesho yaliyofanyika  katika Chumba cha Mifumo ya Kutolea Taarifa Muhimu za Mahakama (Judiciary Situation Room).

Mkurugenzi wa Ukaguzi, Huduma za Mahakama na Maadili wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Maira Kasonde (aliyesimama mbele) akizungumza jambo wakati wa hafla ya kufunga mafunzo elekezi kwa Maafisa wa Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Centre) cha Mahakama juu ya namna ya kuutumia Mfumo mpya wa Utoaji Huduma kwa Wateja (Call Centre Application System).

Sehemu ya Maafisa kutoka Ofisi ya Huduma kwa Mteja ya Mahakama ya Tanzania wakiwa katika hafla fupi ya ufungaji wa mafunzo elekezi juu ya mfumo mpya wa ushughulikiaji wa mirejesho iliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 25 Julai, 2024. 


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya (wa sita kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Maafisa wa Mahakama ya Tanzania mara baada ya kufunga mafunzo elekezi ya namna ya kuutumia mfumo mpya wa ushughulikiaji wa mirejesho yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 25 Julai, 2024.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni