Jumamosi, 27 Julai 2024

MLUNDIKANO WA MASHAURI HAUNA NAFASI KATAVI

Na Innocent Kansha – Mahakama, Katavi

Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Katavi pamoja na Mahakama zake za Wilaya za Mlele, Mpanda na Tanganyika zimeendelea kuonyesha rekodi nzuri katika kuhakikisha zinashughulikia na kukabiliana na mashauri mlundikano yenye mamlaka na yasiyo na mamlaka hadi kufikia Julai, 2024 kulikuwa na mlundikano wa shauri moja (1) tu.

Aya yamesemwa jana tarehe 26 Julai, 2024 na Afisa Utumishi Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Bw. Ayubu Nyallobi kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Bw. Allan Mwella wakati akifanya mazungumzo katika ziara ya Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania Bw. Gerald Chami alipofika ofisini hapo kujitambulisha.

“Katika kipindi cha kuanzia Januari, 2024 hadi Julai 2024 Mahakama mkoa wa Katavi imefanya jitihada za kuendesha vikao vikubwa vitatu vya kusukuma mashauri ya jinai na madai kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mahakama za Wilaya Mpanda, Mlele na Tanganyika,” alisema Afisa Utumishi huyo.

Akizunguzia hali ya mashauri kwa ujumla Bw. Nyallobi alisema, kuanzia mwezi Januari hadi Julai, 2024 Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi ilivuka mwaka 2023 ikiwa na shauri 10, imefanikiwa kusajili mashauri 33, mashauri yaliyoamuriwa 23 na mashauri 20 yanaendelea kusikilizwa.

Kwa upande wa Mahakama ya Wilaya Mpanda ilivuka mwaka 2023 na mashauri 199 na katika cha kuazia Januari hadi Julai, 2024 mashauri yaliyosajiliwa ni 819, mashauri yaliyosikilizwa 852 na yaliyobaki mahakamani ni mashauri 166.

Mahakama ya Wilaya Mlele ilivuka mwaka 2023 na mashauri 24 na katika cha kuazia Januari hadi Julai, 2024 mashauri yaliyosajiliwa ni 197, mashauri yaliyosikilizwa 195 na yaliyobaki mahakamani ni mashauri 26.

Bw. Nyallobi aliongeza kuwa, Mahakama ya Wilaya Tanganyika ilivuka mwaka 2023 na mashauri 85 na katika cha kuazia Januari hadi Julai, 2024 mashauri yaliyosajiliwa ni 291, mashauri yaliyosikilizwa 319 na yaliyobaki mahakamani ni mashauri 57.

Aidha, Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi imekuwa ikipokea idadi ya wateja wengi kwa wastani tofauti tofauti kwa mwezi mfano, katika kipindi cha mwezi Januari, 2023 idadi ya wateja waliopokelewa walikuwa 243 ikilinganishwa Januari, 2024 idadi hiyo ilikuwa 215.

Kwa upande wa mwezi Februari, 2023 wateja waliohudumiwa walikuwa 457 ikilinganishwa na februari, 2024 idadi hiyo ilikuwa ikishabihiana kwa kwa karibu kwa kuhudumia wateja 479. Hii ni kutokana na wananchi wengi kufungua mashauri mahakamani kutokana na msimu wa kuvuna mazao mbalimbali na kuongeza kwa shughuli za kibiashara.

Bw. Nyallobi aliongeza kuwa idadi ya wateja wanaopokelewa huanza kupungu kuanzia miezi ya Machi mfano, Mwezi Machi, 2023 Mahakama ilipokea wateja 362 ikilinganishwa na mwezi Machi, 2024 ambapo jumla ya wateja 345 walipokelewa na kupata huduma za kimahakama. Tafsiri yake ni kwamba shughuli za kiuchumi hasa kupitia sekta ya kilimo huaza kupungua.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi ilianzishwa mwaka 2014, Mahakama hii inajukumu la kusimamia Mahakama za wilaya tatu (3) ambazo ni Mahakama ya Wilaya Mpanda, Mlele na Tanganyika. Pia inasimamia Mahakama za Mwanzo 10 ambazo ni Mpanda Mjini, Katumba, Shanwe zilizoko wilaya ya Mpanda, Inyonga, Usevya, Majimoto zilizoko Wilaya Mlele na Kabungu, Karema, Mwese na Mishamo zilizoko wilaya ya Tanganyika.

Afisa Utumishi Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Bw. Ayubu Nyallobi (Mwenye Kaunda Suti ya Dark Bluu) kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Bw. Allan Mwella akifanya mazungumzo wakati wa ziara ya Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania Bw. Gerald Chami alipofika ofisini hapo kujitambulisha jana tarehe 26 Julai, 2024.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania Bw. Gerald Chami (aliyenyoosha mkono) akiwa na timu ya ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki linaloendelea kujengwa mkoani Katavi  jana tarehe 26 Julai, 2024.

Muonekano wa Jengo la Kituo Jumuishi cha Utaji Haki kinachojengwa mkoani Katavi kwa sasa.
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Mahakama ya Tanzania Bw. Gerald Chami (aliyenyoosha mkono) akiteta jambo na timu ya ujenzi wa kituo hicho.



Muonekano wa Jengo la Kituo Jumuishi cha Utaji Haki kinachojengwa mkoani Katavi kwa sasa.

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

 

 

 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni